Azam FC yampata mrithi wa Himid Mao

Himid Mao

AZAM imepanga kuwatumia viungo wake, Bryson Raphael, Frank Domayo na Abdallah Masoud kuziba nafasi ya nahodha wao, Himid Mao, ambaye anakaribia kujiunga na Bidvest Wits ya Afrika Kusini.

Mao tayari amefanya mazungumzo ya awali na Bidvest, lakini akarejeshwa nchini ili kwenda kuitumikia Kilimanjaro Stars katika michuano ya Chalenji nchini Kenya, ambapo ikimalizika atarejea tena Afrika Kusini kumalizia dili lake.

Meneja wa Azam, Philip Alando, alisema hata kama Mao ataondoka hawatafanya usajili kwani wana wachezaji hao watatu pamoja na Mkameruni, Stephan Kingue ambao wataziba nafasi yake.

“Tutawatumia hao tulionao kwa sasa kwani wanaweza kuziba nafasi yake kwa ufasaha, tuna viungo wengi kwenye timu yetu,” alisema Alando aliyewahi kuzichezea Azam na Toto Africans enzi zake.

“Tunamheshimu Himid Mao kama nahodha wetu na mchezaji mwenye kiwango kikubwa, lakini tunamuombea afanikiwe. Tusingependa kuona anamalizia maisha yake ya soka hapa Chamazi,” alisema.