Azam, Kagera wamalizana Mbaraka ruksa

Dar es Salaam. Mshambuliaji wa Azam, Mbaraka Yusuf aliyewekewa pingamizi la usajili Kagera Sugar amepewa ruksa ya kuitumikia timu yake mpya kwa msimu huu wa Ligi Kuu Bara.

Mbaraka aliwekea pingamizi (TFF), na Uongozi wa Kagera Sugar kuwa bado anamkataba na timu hiyo wa miaka mitatu na Azam wamemsajili kimakosa mshambuliaji huyo.

Ofisa habari wa Azam Jafari Iddi 'Maganga' alisema kuwa jana Alhamisi walikaa kikao na uongozi wa Kagera Sugar makao makuu ya klabu hiyo yaliyopo Mzizima Jijini hapa Dar es Salaam, na kufikia muafaka juu ya mshambuliaji huyo.

Maganga alisema kuwa kikao na uongozi wa Kagera Sugar yalikwenda sawa na wametoa ruksa na kumluhusu mshambuliaji huyo kuanza kuitumikia timu yake mpya na wamemtakia kila la heri.

"Uongozi wa Kagera Sugar umekubaliana na Azam na kutoa ruksa mchezaji huyo kuwa na timu yake mpya ya Azam na uongozi huo utakwenda kufuta pingamizi ambalo waliliweka hapo awali juu yake pale TFF," alisema.

Mbaraka msimu uliopita alifunga mabao mengi kuliko washambuliaji Donald Ngoma, Amiss Tambwe wa Yanga, na Laudit Mavugo wa Simba.

Maganga alisema kuwa Azam baada ya kumaliza maandalizi ya msimu mpya huko Uganda watacheza mechi ya mwisho ya kirafiki dhidi ya timu yao ya vijana na baada ya hapo watakwenda Mtwara Agasti 23, siku mbili kabla ya kuwavaa Ndanda katika mechi ya kwanza ya Ligi Kuu Bara.