Arsenal yakutana na ratiba chungu

Muktasari:

  • Tottenham iliyoziengua Chelsea na Arsenal katika ‘top four’ ikitamba kwa msimu wa tatu mfululizo licha ya kujadiliwa sana kutokana na kutosajili mchezaji yeyote katika dirisha la usajili wa kiangazi, lakini imethitisha kuwa haikuwa na sababu za kusajili kwani inacho kikosi bora baada ya kushinda ugenini kwa mabao 2-1 dhidi ya Newcastle United.

London, England. Kinyang’anyiro cha Ligi Kuu England, kimeanza tangu wikiendi iliyopita, timu zinazotabiriwa kumaliza ndani ya nne bora, mabingwa watetezi Manchester City, Liverpool, Tottenham na Manchester United zikianza kwa kishindo.
Tottenham iliyoziengua Chelsea na Arsenal katika ‘top four’ ikitamba kwa msimu wa tatu mfululizo licha ya kujadiliwa sana kutokana na kutosajili mchezaji yeyote katika dirisha la usajili wa kiangazi, lakini imethitisha kuwa haikuwa na sababu za kusajili kwani inacho kikosi bora baada ya kushinda ugenini kwa mabao 2-1 dhidi ya Newcastle United.
Ujio wa Kocha, Maurizio Sarri, unaweza kuwa suluhisho kwa Chelsea, kwani aliiwezesha kushinda mabao 3-0 dhidi ya timu ngeni katika Ligi hiyo, Huddersfield Town, lakini wikiendi hii ndipo atapaswa kuthibitisha kama anao ubavu wa kuchuana kuing’oa Tottenham ndani ya nne bora.
Sarri atathibitisha hilo, atakapoiongoza Chelsea kuikaribisha Arsenal kwenye Uwanja wa Stamfodge Bridge, iwapo itaondoka na ushindi wa kishindo kama ilioupata kwa Huddersfield ataanza kuwashawishi wengi kuipa nafasi ya kufanya vema msimu huu.
Arsenal jana Jumapili iliyopita ilicheza mechi yake ya kwanza ya ushindani bila Arsene Wenger kwa mara ya kwanza tangu mwaka 1996, licha ya kuwa nyumbani kocha Emery Unai hakuweza kuiepusha na adhabu kutoka kwa mabingwa watetezi City na kufungwa mabao 2-0.
Kocha wa kuwa huyo wikiendi ijayo pia atakuwa katika wakati mgumu kwani atasafiri kuifuata Chelsea moja ya timu ambazo zinaonekana zina vikosi bora vinavyoweza kupigania ubingwa.
Kwa upande wake Kocha City, Pep Guardiola alitamba kuwa kikosi chake kitazidi kutoa dozi kwa kila timu itakayocheza nayo akidai timu hiyo inamarika siku hadi siku.
Guardiola alisema kuwa anaamini katika mechi ijayo sio Bernardo Silva na Raheem Sterling pekee walioifungia mabao hayo, watakafunga tena wikiendi ijayo bali wafungaji wataongezeka watakapoikaribisha Huddersfield Jumapili hii.
Nayo Manchester United chini ya Jose Mourinho imeanza vema Ligi baada ya kuichapa timu bingwa ya Ligi hiyo msimu wa 2015/16, Leicester City kwa mabao 2-1 na wikiendi hii itaifuata timu isiyo na uzoefu ya Brighton.
Upande mwingine, Henrikh Mkhitaryan aliyehamia Arsenal akitokea United pamoja na washambuliaji mahiri Pierre-Emerick Aubameyang na Alexandre Lacazette hawakuibeba Arsenal kama walivyofanya katika timu zao za zamani Aubameyang alikua tegemeo la mabao kwa Borussia Dortmund ya Ligi Kuu Ujerumani ‘Bundesliga’ na Lyon ya Ufaransa ‘Ligue 1’.
City ambayo iliilaza Chelsea mabao 2-0 katika mchezo wa Ngao ya Jamii inaonekana kuzidi kuimarika kila kukicha na sasa ni wazi kuwa inaweza kuandika historia ya kuwa timu ya kwanza kutetea taji la Ligi Kuu.
City iliyomnunua Riyad Mahrez pekee katika dirisha la usajili wa kiangazi kwa Pauni 60 milioni kutoka Leicester City, alionyesha ana kitu amekiongeza kwa City.
Mitambo ya Liverpool inaonekana imeongezeka nguvu na imeonyesha dalili kuwa itaangamiza zaidi msimu huu baada ya Sadio Mane kufunga mawili, Mohamed Salah na Daniel Sturridge nao wakitupia, huku James Milner na Robeto Firmino, wakicheza soka la kiwango cha juu, hata hivyo Liverpool wikendi hii itakuwa ugenini ikiifuata Crystal Palace.