MTAA WA KATI: Angalau sasa nimeanza kumwelewa Jose Mourinho

Said Pendeza

SASA nimemwelewa Jose Mourinho. Mara zote nimekuwa nikimnyoonyeshea kidole Man United inapocheza ovyo na kupata matokeo yasiyoendana na hadhi yao. Lakini, sasa nimegundua ni suala la kisaikolojia zaidi. Kuna wanaoamini kwamba Mourinho ameishiwa mbinu.

Wanaoamini ule mpira wake hauna maana tena siku hizi. Lakini, hilo haliwezi kutazamwa tu kwa matokeo ya msimu huu.

Mourinho hajazidi miaka mitatu tangu alipobeba ubingwa wa mwisho wa Ligi Kuu England. Mwaka jana aliwapa Man United Europa League na Kombe la Ligi. Achana na Ngao ya Jamii. Yawezekana Man United imefanya usajili wa pesa nyingi, lakini tatizo kubwa linalowasumbua ni saikolojia ya wachezaji. Hilo linatokana na rekodi zao kwa miaka ya karibuni.

Man United imekumbwa na athari za kisaikolojia tu.

Kwa miaka ya karibuni, wamekuwa si tishio tena tangu alipoondoka Sir Alex Ferguson.

Kosa kubwa lililofanywa ni kwamba ilimbadili Ferguson kwa kocha wa kiwango cha chini sana, David Moyes.

Ukweli usiopingika, Moyes hakuwa na hadhi ya kurithi mikoba ya Ferguson.

Tangu hapo timu ilibadilika na rekodi kibao zilivunjwa. Man United ilipoteza hadi na timu ambazo hazikudhaniwa itatokea siku zitapata matokeo ya ushindi dhidi ya timu hiyo, tena kwenye Uwanja wa Old Trafford.

Wapinzani wakaanza kujiamini wanapocheza dhidi ya Man United, kwamba wanafungika. Jambo hilo limeingiza hofu ya moja kwa moja Man United kwamba wao si tishio tena.

Hilo likawafanya wawe wameathirika kwa kiasi kikubwa.

Akaletwa Louis van Gaal, akashindwa kurudisha ile nguvu ya Man United, waliendelea kuwa dhaifu. Wamekuwa si timu ya kuwakimbiza wenzao, ni wao sasa ndio wanaokimbizwa, tena hufanywa hivyo hadi na timu dhaifu.

Man United imegeuka kuwa timu ya kukaba na si kukabwa. Hilo limewaathiri sana kisaikolojia, ambalo ndilo hasa linalowaandama hadi sasa.

Rekodi zao za miaka ya karibuni, zinatosha kuwafanya Man United kuwa na hali kama hiyo. Ubingwa wao wa mwisho kwenye Ligi Kuu England ulikuwa msimu wa 2012/13.

Baada ya hapo, nafasi kubwa waliyowahi kushika kwenye Ligi Kuu ni namba nne.

Zaidi ya hapo wameshakuwa nafasi ya saba, sita na tano. Jambo hilo linafanya ile nguvu ya kuamini kwamba wao ni Man United imeondoka.

Hilo moja, mbili ni wachezaji pia waliokuwapo kwenye timu hiyo. Wengi walikuwa wa viwango vya kawaida sana.

Man United ilifikia hatua ya kumtegemea mchezaji kama Adnan Januzaj.

Man United ya kumtegemea Jesse Lingard au Marcos Rashford? Hao ni wachezaji wa kuchezeshwa kwenye mechi za Kombe la FA, Kombe la Ligi na si panga pangua kuwategemea hadi kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya au Ligi Kuu England.

Walipaswa kucheza mechi moja moja sana, si kuwa tegemeo. Hiyo ndiyo Man United ambayo ameithiri Mourinho.

Ipo chini kisaikolojia na haikuwa na wachezaji wa maana.

Anachokifanya Mourinho ni kujaribu kuleta wachezaji watakaobadili saikolojia iliyopo.

Kuleta wachezaji watakaoirudisha hadhi ya Man United, japo si kitu kinachoweza kufanyika ndani ya usiku mmoja.

Kuirudisha ile nguvu yao ya miaka ya nyuma inahitaji subira ya muda mrefu.

Pengine hata kipindi cha Mourinho kikapita na kuja kocha mwingine.

Chini ya Moyes ilipoteza hadi hadhi ya kusajili wachezaji wa maana.

Toni Kroos, Cesc Fabregas, Thiago Alcantara ni wachache tu waliokataa kuja kujiunga na Man United iliyokuwa chini ya Moyes.

Man United haikuwa ileile tena.

Mourinho ndiye wakuirudisha timu hiyo kwenye hadhi yake, bado ana nguvu ya ushawishi kwa wachezaji wa kiwango cha dunia wakachagua kuja kujiunga na Man United.

Wachezaji wanaomfahamu Mourinho wanatambua wazi, ukipiga kazi na kufuata kile anachokielekeza, huwezi kuwa adui yake.

Mourinho anataka wapiga kazi na si matozi.

Mpira wa sasa umebadilika, una kipaji sawa, lakini unapaswa kukifanyia kazi kipaji ulichonacho.

Man United inahitaji wachezaji wa maana zaidi.

Hata mabosi wa timu hiyo wanafahamu wazi na ndio maana hawasiti kutoa pesa inapohitajika kufanya hivyo, wanatambua timu yao inahitaji kuwa na wachezaji wenye uwezo na si kutegemea beki ya Chris Smalling.

Man United hii ukichekacheka, itakufia zaidi, inahitaji kocha mkali kama Mourinho, ambaye haogopi kumweka benchi mtu kama Pogba, ambaye kitu kinachobadilika kutoka kwake ni mitindo ya nywele tu kutoka mechi moja hadi nyingine.