Ancelotti kupewa mikoba ya Wenger

Muktasari:

Mkataba wa sasa wa kocha Wenger (68) una kipengele kinachoruhusu kufanyiwa tathmini namna timu ilivyofanya kwa msimu huu na kama kutakuwa na mambo yasiyofurahisha, basi atalazimika kumpisha mtu mwingine kwenye kiti.

MILAN, ITALIA

NDIYO wanavyosema kuwa Carlo Ancelotti amekubali kwenda kuchukua mikoba ya Arsene Wenger huko Arsenal wakati msimu huu utakapofika tayari, zinafichua ripoti za kutoka Italia.

Ikifika mwisho wa msimu, Wenger atakuwa bado ana mkataba wa mwaka mmoja wa kuendelea kuinoa Arsenal, lakini mambo yatakuwa tofauti kabisa kama Washika Bunduki hao wa Emirates watamaliza msimu mikono mitupu.

Mkataba wa sasa wa kocha Wenger (68) una kipengele kinachoruhusu kufanyiwa tathmini namna timu ilivyofanya kwa msimu huu na kama kutakuwa na mambo yasiyofurahisha, basi atalazimika kumpisha mtu mwingine kwenye kiti. Makocha kadhaa wameanza kuhusishwa na kiti hicho cha Wenger akiwamo Thomas Tuchel, Eddie Howe na Sean Dyche na siku za karibuni, Mikel Arteta.

Lakini, Corriere dello Sport linaripoti kwamba Arsenal wao wameshafikia makubaliano na Ancelotti kwa ajili ya kuwa kocha wao mwisho wa msimu. Mtaliano huyo ambaye aliwahi kuinoa Chelsea atasaini mkataba wa miaka minne wenye thamani ya Pauni 8.7 milioni kwa mwaka na bonasi nyingine kibao. Ripoti zaidi zinadai kwamba, Ancelotti atakwenda London mwezi ujao. Taarifa nyingine zinadai kwamba Shirikisho la Soka la Italia linamshawishi Ancelotti akatae ofa ya Arsenal ili kupewa kazi ya kuinoa timu ya taifa ya Italia, Azzurri. Ancelotti, 58, kwa sasa hana kazi tangu alipofukuzwa na Bayern Munich, Septemba mwaka jana.