Amunike kocha mpya Taifa Stars

Dar es Salaam.Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) limemtangaza mshambuliaji wa zamani wa Nigeria, Emmanuel Amunike kuwa kocha mkuu mpya wa Taifa Stars.

Rais wa TFF, Wallace Karia amemtangaza Amunike kocha wa zamani wa timu ya vijana ya Nigeria kuwa mrithi wa Salum Mayanga.

"Tumeingia mkataba wa miaka miwili na Amunike utakuwa na nyongeza mbele kama itayafanya yake ambayo tumekubaliana katika mkataba wetu," alisema Karia.

"Atakuwa kocha wa Taifa Stars na timu za vijana chini ya umri wa miaka 17, 20 na 23 na atakuwa na kocha wake msaidizi.

"Katika benchi la ufundi pia kutakuwepo na kocha mzawa ambaye atakuwa akifanya kazi kwa kusaidiana nao, " alisema Karia.

Naye Amunike alisema nchi nyingi za Afrika zinawachezaji wengi wazuri ila wanakosa maandalizi ya msingi ambayo yanawafanya kushindwa kufanya vizuri.

"Naomba ushirikiano kuanzia kwa viongozi na wote ambao wanahusika na timu ili kufanya vizuri na kupiga hatua katika soka la Tanzania," alisema Amunike.