Amsha amsha ya Simba na Yanga

Muktasari:

  • Kwa wiki nzima Mwanaspoti limekuwa likitembelea matawi ya klabu hizo ili kupata mawili matatu kutoka kwa mashabiki na safari hii tumewazukia wanachama wa Yanga Tawi la Tandale Umoja pale Kwa Mtogole na lile la Simba la Mpira na Maendeleo a.k.a Simba Ukawa.

 ZIMEKATIKA mwanangu! Ile siku iliyokuwa inasubiriwa kwa hamu ya pambano la watani wa jadi, Simba na Yanga imewadia wakati vigogo hivyo vitakaposhuka uwanjani kupepetana kwenye Uwanja wa Taifa, jijini Dar es Salaam leo Jumamosi.

Kwa wiki nzima Mwanaspoti limekuwa likitembelea matawi ya klabu hizo ili kupata mawili matatu kutoka kwa mashabiki na safari hii tumewazukia wanachama wa Yanga Tawi la Tandale Umoja pale Kwa Mtogole na lile la Simba la Mpira na Maendeleo a.k.a Simba Ukawa.

Unajua wamesema yepi? Wasikieni wenyewe kuelekea mtangane wa timu zao;

MNYAMA ANAKUFA  MAPEMAAA

Wanachama wa Yanga wa Tandale Umoja wanaamini kuwa wameshaifunga Simba mapema nje ya uwanja.

Mohamed Kagari mwenye kadi namba  009888, alisema Simba inakufa 2-0 tena dakika 45 za awali.

“Siku zote nanunua tiketi ya Sh.7000 lakini awamu hii nimenunua ya Sh.30000 kwa sababu najiamini naenda kukaa kwenye majukwaa ya waheshimiwa sitaki kushangilia kwa kumwagiana maji maana najua tumeshinda sehemu zote.”

Naye Felix Mwambembule mwenye kadi namba 093, alisema Simba haichomoki kwani watagongwa tatu na huenda Abdi Banda, Lufunga ama Bukungu kulimwa kadi nyukundu.

“Walikoweka kambi Yanga, kuna historia ya ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya Simba, ilikuwa ni mwaka 1999 ndiyo maana tunajiamini kwamba hawatatoka na mashabiki wao wa mtaa huu wamekata tamaa ya kwenda uwanjani,” alisema.

HAO YANGA HAWACHOMOKI

Wanachama wa Simba maarufu kama ‘Simba Ukawa’ waliposikia tambo za Yanga wakacheka sana na kutamka kwa upole walahi Yanga watalala mapema maana safari hii hawatoki salama.Katibu Mkuu wa tawi hilo la Mpira na Maendeleo linalounda Simba Ukawa, Mbalike Salum alisema kikosi chao kwasasa kimeimarika tofauti na mwanzo hivyo kuna asilimia kubwa ya kupata ushindi mapema.

“Ukiangalia kikosi cha Simba kipo imara sana kipindi hiki, mabeki wapo vizuri na hata washambuliaji wanaelewana ndiyo maana idadi ya magoli kwenye mechi za hivi karibuni imeongezeka. Yanga wamechoka.” “Tuliacha kuishangilia  kama kundi,  kila mmoja huwa anaenda uwanjani kutoa sapoti. Bado tunaombolewa wenzetu waliotangulia mbele ya haki.”