Amsha amsha ya Simba na Yanga

HUKU visiwani joto la pambano la watani limefikia mahala pake, wanachama na mashabiki wa klabu hizo wakipigana vijembe ikiwa ni saa chache kabla ya timu zao kesho Jumamosi kushuka Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kuonyeshana ubabe.

YANGA HAINA CHAO

Mashabiki wa Simba matawi ya Amaan, Kariakoo mjini Unguja, wametamba kuwa Yanga haina chao kwao ni lazima walale mapema. “Yanga wanatambua kabisa kuwa sisi (Simba) hatuna masihara na ushindi ni lazima,” alisema Said Hamza.

Hassan Alawi alifichua kama Yanga wanadhani watatoa salama pengine Simba kuna mgogoro, wameumia kila kitu Msimbazi sasa ni shwari.

Mwenyekiti wa matawi ya Simba Zanzibar, Issa Ahmada ‘Jogoo’ alisema; “Kwa mziki huu unaoendelea kupiga tizi hapa, Yanga wala wasisumbuke hata kufanya mazoezi wanajichosha bure kwani kipigo kipo palepale.”

Jogoo alisisitiza kuwa faida ya kambi kwa timu yao hiyo visiwani Zanzibar si kwa mchezo kati yetu na Yanga tu, bali ni kwa michezo yote inayotukabili katika kukamilisha ligi kuu Tanzania bara msimu huu .

JIDANGANYENIMUUMIE

Yanga waliposikia tambo za watani zao wakacheka sana, kisha wakasema kwa kujiamini, watani nyie jidanganyeni muumie Taifa.

Wanachama na mashabiki wa tawi la Mwanakwerekwe, wakiongozwa na Jamal Ali walisema kuwa Simba hawezi kupona kesho kwani anaamini kila kitu kipo freshi kwao, huku akiapa kuacha kila kitu chake kesho ili kufuatilia mchezo huo.

Naye Khamis Khalid, alisema yeye hawezi kusema bila ya vitendo, hivyo anafunga safari toka Unguja kuja Dar es Salaam ili kushuhudi mnyama akifa mubashara mbele yake.

Mwenyekiti wa matawi ya Yanga Zanzibar, Samir Masoud ‘Ankosami’, alisisitiza kuwa Wanayanga hawana mchecheto kabisa na Simba kwa kujua kuwa ni lazima wamlambishe mchanga mapema.

Alisema kelele za mashabiki wa Simba kuifunga Yanga ni kujidang’anya ila wanajua lazima waumie Taifa.