Amsha amsha kambi ya Simba si mchezo

KAMBI ya Simba huko Afrika Kusini imenoga si mchezo, lakini Kocha Mkuu wa timu hiyo, Mkameruni Joseph Omog,  amesema kiungo Haruna Niyonzima akitua tu kambini hapo itakuwa balaa zaidi.

Omog anayewanoa vijana wake katika kambi hiyo iliyoanza wikiendi iliyopita, ameliambia Mwanaspoti kuwa kikosi chao kinafanya mazoezi mara mbili kwa siku baada ya kumaliza programu ya wiki moja ya kuandaa miili ya nyota wake.

Kocha Omog alisema aliwafanyia amsha amsha nyota wake waliokuwa wanatoka mapumzikoni, lakini kwa sasa ameanza programu ya pili kwa ajili ya utimamu wa mwili na akili pamoja na ufundi ili kuwajenga kwa ajili ya msimu mpya.

AMTAJA  NIYONZIMA

Kuna tetesi kuwa Niyonzima aliyeichezea Yanga kwa takribani miaka sita, amesaini Simba, kuhusu hilo Omog alisema: “Sina ninachojua kuhusu Niyonzima, ila ni mchezaji mzuri ambaye hakuna kocha anayeweza kumkataa. Ana kipaji na kama atatua kwetu mambo yatakuwa mazuri zaidi.”

Mwanaspoti linafahamu kuwa mkataba wa Niyonzima Yanga unamalizika leo Ijumaa na kesho anaweza kwenda Sauzi kuungana na wenzake kambini.