Safu ya ushambuliaji yamvuruga kocha wa Alliance Qeen

Muktasari:

  • Timu hiyo ya jijini Mwanza, imevuna pointi saba na kukaa nafasi ya tatu kwenye msimamo wa ligi hiyo.

 Kocha wa Alliance Queen, Ezekiel Chobanka amesema kuwa kwa kipindi hiki ambacho Ligi Kuu ya Wanawake imesimama, atatumia muda mwingi kurekebisha mapungufu katika safu ya ushambuliaji ili kujiweka kwenye vita ya ubingwa.

Timu hiyo ya Jijini Mwanza, imevuna pointi saba na kukaa nafasi ya tatu kwenye msimamo wa Ligi hiyo inayoongozwa na vinara JKT Queen wenye alama 12 baada ya kucheza mechi nne kila mmoja.

Kocha Chobanka alisema kuwa katika kuhakikisha wanawania ubingwa, atapambana  kwa nguvu kuisuka vyema safu ya ushambuliaji ili kila mchezo wapate mabao ya kutosha.

Alisema kuwa licha ya mapungufu mengine yaliyopo kama eneo la beki,lakini kubwa anahitaji safu ya umaliziaji ikae sawa, kisha maeneo mengine yafuate.

“Ushindi wowote huwa ni mabao, hata hao JKT wanaoongoza ni kwa sababu walishinda kwa kufunga mabao, hivyo na mimi kwa muda huu nitahakikisha safu ya ushambuliaji inakaa sawa,” alisema Chobanka.

Aliongeza kuwa matarajio yake ni kuisaidia timu kutwaa ubingwa na kwamba uwezo wa vijana wake ndio unampa kiburi cha kutamba kufanya kweli.

Alisema kuwa licha ya ushindani uliopo kwa timu pinzani, lakini hana wasiwasi na kwamba lazima awashushe JKT na Sisters walioko juu yake.