Ali Kiba kumbe yupo Coastal kikazi zaidi

Muktasari:

  • Awali usajili wa Kiba kwa Wagosi uliamsha hisia za mashabiki wa soka nchini baada ya kuona msanii huyo akiingia moja kwa moja kwenye soka licha ya dili zake kibao za muziki zikimuingizia mkwanja wa maana na kumpaisha ndani na nje nchi.

ALIKIBA mjanja sana, kwani licha kusaini mkataba ili kukipiga kwa mabingwa hao wa zamani wa Tanzania, lakini kumbe ameweka mzigo maana mezani ili kuidhamini klabu hiyo kupitia kinywaji chake cha Mo Faya.

Habari kutoka ndani ya Coastal zinasema kuwa, Kiba na Wagosi wameingia makubaliano ya kibiashara yenye thamani ya Sh100 milioni ikiwa ni udhamini wake kwa klabu hiyo kupitia kinywaji chake hicho.

Awali usajili wa Kiba kwa Wagosi uliamsha hisia za mashabiki wa soka nchini baada ya kuona msanii huyo akiingia moja kwa moja kwenye soka licha ya dili zake kibao za muziki zikimuingizia mkwanja wa maana na kumpaisha ndani na nje nchi.

Mwanaspoti baada ya kunusa taarifa hizo liliwatafuta baadhi ya vigogo ndani ya klabu hiyo (Jina linahifadhiwa), ambapo alikiri kwamba kuna makubaliano maalumu katika pande zote mbili, Kiba na Coastal Union, japo hakutaka akishindwa kuweka.

“Awali kulikuwa na dili hilo la mkwanja lakini baadaye tulikaa chini na kuzungumza pande zote mbili na kukubaliana baadhi ya vitu, Kiba ni jina kubwa lakini hapa amesajiliwa bila pesa ndio maana kuna makubaliano yaliyopo kimkataba,” alisema kigogo huyo.

Aliendelea kwa kusema kwamba sehemu ambayo wameambulia pesa ni kupitia jezi zao baada ya kuweka wadhamini kampuni ya Binslum, TSN pamoja na GSM katika udhamini wao.

“GSM wametoa Sh 40 milioni, TSN wao wameweka 30 milioni na BinSlum ametoa Sh 75 milioni, lakini vile vile kupitia jezi hizi za Bongo tunazovaa tutakuwa tunapata pesa kwa jinsi ambavyo zitauzwa na sisi ndio tunaingiza,” alisema.

Imedaiwa, uongozi wa Coastal haupendi kuanika wazi udhamini wa Kiba pamoja na masuala mengine yanayomhusu msanii huyo kwasababu Kiba hapendi mambo yake kuwekwa hadharani.

Upande wa Kiba hakupenda kuzungumza suala la udhamini wake, ila alisema

‘’Nina furaha kuanza kukifanyia kazi kitu ambacho nakihusudu sana baada ya muziki wangu. Naishukuru Costal Union kwa kuniamini na kuungana nami kupitia brand yangu ya Mo Faya Energy Drink na kunipa fursa ya kuwa sehemu ya timu.”

Alikiba alisema ushirikiano baina ya pande mbili yaani klabu na yeye utaleta mafanikio kwa wote.