Ajibu katua Yanga tu, Simba...

Muktasari:

Mchecheto huo ndio uliowafanya waamue kufanya usajili wa mabeki tisa na makipa watano ili kuweza kuzima nguvu zao, hasa katika pambano la Ngao ya Jamii litakalopigwa Agosti 23 jijini Dar es Salaam.

YANGA imemsajili yule kiberenge aliyekuwa aende Lipuli ya Iringa, lakini sasa kama hujui, straika Ibrahim Ajibu aliyetua Jangwani kutoka Simba, ameitikisa timu yake ya zamani kiasi cha kufikia kusajilia mabeki tisa na makipa watano ili kumzuia asiwaaibishe.

Kutua kwa Ajibu ndani ya Yanga na kuungana na safu yenye wachana nyavu hatari wakiongozwa na Amissi Tambwe, Donald Ngoma na Obrey Chirwa waliofunga jumla ya mabao 31 kati ya 57 ya msimu uliopita,  kumewafanya viongozi wa Simba na benchi lao la ufundi kuingiwa na mchecheto mkubwa.

Mchecheto huo ndio uliowafanya waamue kufanya usajili wa mabeki tisa na makipa watano ili kuweza kuzima nguvu zao, hasa katika pambano la Ngao ya Jamii litakalopigwa Agosti 23 jijini Dar es Salaam.

Rekodi zinaonyesha kwamba Yanga ndiyo klabu iliyoweza kufunga mabao mengi zaidi Ligi Kuu katika misimu miwili mfululizo, ambapo msimu wa 2015/16 ilifunga mabao 70 kabla ya kufunga mabao 57 msimu uliopita.

Hofu hiyo ya Yanga kutikisa zaidi mabao imewafanya Simba kuweka nguvu kubwa katika usajili wa nyota hao 14 wa safu ya ulinzi. Mabeki wapya ambao tayari wamejiunga na Simba sasa ni Shomary Kapombe na Erasto Nyoni kutoka Azam, Yusuf Mlipili kutoka Toto Africans na Ally Shomary na Salim Mbonde kutoka Mtibwa Sugar. Mwingine ni Jamal Mwambeleko kutoka Mbao FC.

Nyota hao wanaungana na Method Mwanjali, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ na Juuko Murshid na kufanya mabeki wa Wekundu wa Msimbazi kuwa tisa.

Mbali na mabeki, Simba imewasainisha pia kipa bora wa Ligi Kuu mara mbili mfululizo, Aishi Manula, kipa bora wa Cosafa, Said Mohammed ‘Nduda’ na Emmanuel Mseja kutoka Mbao FC. Makipa hao wanaungana na Denis Richard na Manyika Peter ambao walikuwapo japo kuna tetesi huenda wakatolewa kwa mkopo, hapo bado hujamtaja Mghana Daniel Agyei anayeelekea kutemwa kikosini. Na hapo bado wanaendelea na usajili mpaka Agosti 6 dirisha hilo litakapofungwa.

KIBERENGE ASAINI

Jana mchana mabosi wa Yanga walimalizana na Burhan Yahya Akilimali aliyedakwa juu kwa juu wakati akiwania kusajiliwa Lipuli na kumsainisha mkataba wa miaka miwili.

Yahya anayekwenda kwa jina la utani la Kiberenge kutokana na kasi aliyonayo, ametua Jangwani kuchukua nafasi ya Simon Msuva anayejiandaa kutimkia Morocco na amesema anajisikia furaha kutua timu kubwa yenye nyota kama Ajibu, Tambwe na Ngoma na kuahidi kutowaangusha.

“Nimefurahi kutua Yanga na hasa kukutana na Ajibu, naamini tutashirikiana kuipa Yanga mafanikio msimu ujao,” alisema winga huyo aliyekuwa akisoma Uganda na kuonwa na Lipuli wakati wa mechi za Ndondo Cup.

ABDUL AFUNGUKA

Usajili huo wa Simba umemfanya beki Juma Abdul kusema, watani zao ni kama wanajimaliza mapema kwa kukusanya mastaa ambao hajaona kama wanaweza kuibeba mbele ya kikosi cha George Lwandamina.

Abdul alisema usajili uliofanywa na Simba unaweza kuwafurahisha wengi, lakini kwake hajaona kikubwa zaidi ya kukusanya majina makubwa ambayo yanaweza kuwavuruga kutokana na kila mmoja kujiona anajua.

Alisema kosa wanalofanya Simba liliwahi kufanywa na Yanga miaka michache iliyopita kwa kusajili kikosi cha maana kuanzia golini mpaka benchi, lakini bado walilala kwa Wekundu hao.

“Nafuatilia taarifa zao naona wanasajili majina makubwa tu, hilo ni kosa linaloweza kuwagharimu kama wasipokuwa makini,” alisema.