Ajibu, Tambwe mtakoma

Muktasari:

Yanga iliyoondoka asubuhi ya jana Jumatatu itaivaa Gor kesho Jumatano saa moja usiku kwenye Uwanja wa Moi Kasarani kusaka pointi tatu za kwanza kujiweka pazuri katika Kundi D linaloongozwa na USM Alger ya Algeria.

KIKOSI cha Yanga kimetua salama jijini Nairobi huku nyota wake, Ibrahim Ajibu, Yohana Mkomola na Amissi Tambwe, wakijazwa upepo ili kumaliza kazi mapema katika pambano la Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya wenyeji wao Gor Mahia.

Yanga iliyoondoka asubuhi ya jana Jumatatu itaivaa Gor kesho Jumatano saa moja usiku kwenye Uwanja wa Moi Kasarani kusaka pointi tatu za kwanza kujiweka pazuri katika Kundi D linaloongozwa na USM Alger ya Algeria.

Benchi la Ufundi la Yanga limepata hasira na kuwajaza upepo nyota wao ili kuona wanaipa ushindi wa kwanza timu yao ugenini baada ya kusikia tambo za Kocha wa Gor, Dylan Kerr, aliyedai eti lazima wawapige Yanga licha ya uchovu walionao.

Kocha wa Yanga, Mwinyi Zahera na wasaidizi wake, wameiangalia rekodi ya timu yao dhidi ya Gor Mahia na kubaini wanapaswa kushinda mchezo huo ili kujiweka sawa kundini na pia kumnyamazisha Kerr.

Kerr aliyewahi kuinoa Simba, hajawahi kupata ushindi mbele ya Yanga, lakini rekodi zinaonyesha katika mechi tatu za mwisho baina ya timu hizo, Yanga haijawahi kutoka na ushindi zaidi ya kulala mara mbili na mechi moja kumalizika kwa sare.

Unyonge wa Yanga kwa Gor Mahia ulianza mwaka 1996 walipotoka sare ya bao 1-1 katika hatua ya makundi ya Kombe la Kagame kabla ya kukutana tena katika mechi ya kuwania mshindi wa tatu wa michuano hiyo na Yanga kulala mabao 4-0.

Timu hizo zilikutana tena Julai 2015 katika michuano ya Kagame na Yanga kulala tena mabao 2-1, jambo lililomfanya Kocha Zahera kuwasisitizia vijana wake wakae mguu sawa ili washinde mechi ya kesho kuwanyamazisha wapinzani wao.

Kocha Zahera anatarajia kuwatumia Ajibu, Tambwe na Mkomola eneo la mbele ili kupata matokeo, baada ya Obrey Chirwa kukosekana kutokana na kutimkia Misri, lakini akiwategemea akina Juma Mahadhi, Emmanuel Martin na Pius Buswita waliopo kwenye msafara huo ulioondoka saa 3 asubuhi ya jana kwa usafiri ndege.

Mmoja wa viongozi wa Yanga, amemnukuu Zahera akiwataka nyota wake kupata ushindi katika mchezo wa kesho ili kufufua matumaini ya kutinga robo fainali ya michuano hiyo na pia kutuliza mioyo ya Wana Jangwani ambao wamekuwa na msimu mbaya kwani Yanga imepoteza taji la Ligi Kuu na tiketi ya mechi za CAF.

“Kocha amewasisitiza wachezaji wote watakaoanza mchezo dhidi ya Gor Mahia, amewataka wahakikishe wanacheza kwa kushambulia lango la Gor na kulilinda lao ili tushinde mchezo huo,” alisema kiongozi huyo.

“Amewakazania mastraika kuhakikisha wanazitumia nafasi watakazotegengeza, ili tupate mabao mengine na kuibuka na ushindi, pia kuzima ngebe za Kerr ambaye tangu katika Kombe la Kagame, amekuwa akiisema vibaya timu yetu.”

KERR AGWAYA

Nyota wa Yanga washindwe wenyewe tu kesho Nairobi, kwani wapinzani wao watawakabili wakisumbuliwa na uchovu kutokana na kushiriki michuano miwili mikubwa ya SportPesa Super Cup na Kagame na hiyo ni nafasi kwa Yanga kumaliza kazi mapema.

Ndani ya kipindi cha miezi miwili, Gor Mahia imecheza zaidi ya michezo 20 ya Ligi ya Kenya, SportPesa Super Cup, Kombe la Shirikisho, Kagame mbali ya ile ya kirafiki, jambo linalompa hofu Kerr.

“Kimsingi si mechi rahisi, hata kwa Yanga kwani ukiangalia, tuna siku mbili tu za kujiandaa na mchezo huu sidhani kama tutafanya programu nyingi zaidi ya zile nyepesi za kuweka sawa miili ya wachezaji kabla ya kuingia uwanjani kucheza,” alisema Kerr.

“Tumekuwa na michezo mingi mfululizo ambapo ndani ya siku 17 tumecheza mechi tisa jambo ambalo limepelekea wachezaji wangu kuchoka, lakini tutapambana ili kushinda nyumbani.

“Tumerudi Nairobi Jumamosi na ilikuwa lazima niwape nyota wangu angalau siku mbili za mapumziko kupunguza uchovu walionao. Kama tungepata muda wa kutosha wa mapumziko na maandalizi nadhani Yanga wangepata wakati mgumu.”

Pia aigusia ubutu wa safu yake ya ushambuliaji tangu aondoke Meddie Kagere aliyetua Simba, akidai sio jambo la kufurahisha kuona timu inatengeneza zaidi ya nafasi tisa halafu inafunga mabao mawili au moja, hata hivyo bado naamini wana nafasi kubwa ya kuifunga Yanga.

“Ningepata wasiwasi mkubwa kama tungekuwa hatutengenezi nafasi kwani muda wa kufanyia kazi hilo ungekuwa hautoshi, ila kwa vile tumekuwa tukitengeneza nafasi, naamini tutaweza kufanya vizuri Jumatano,” aliongeza Kerr

Kikosi YANGA

kinaweza KUWA;

Rostand, Abdul, Mwinyi, Ninja, Dante, Tshishimbi, Mahadhi, Buswita, Tambwe, Ajibu na Martin.