Yanga yaichakaza Stand United

Muktasari:

  • Yanga na Simba sasa zitakutana Oktoba 28 kila moja ikiwa imeshinda mabao manne katika mechi yake ya mwisho

Shinyanga. Nyota ya mshambuliaji wa Yanga, Ibrahim Ajib imezidi kung'aa baada ya kufunga mabao mawili na kuingoza timu yake kuichakaza Stand United kwa mabao 4-0 kwenye Uwanja wa Kambarage, Shinyanga.

Ushindi huo wa Yanga umeifanya kufikisha pointi 15, sawa na watani zao Simba wakiongoza ligi kwa tofauti ya mabao kabla ya mchezo baina yao utakaofanyika Jumamosi ijayo kwenye Uwanja Uhuru, Dar es Salaam.

Ajib ameendelea kuwaonyesha Yanga kuwa hawajakosea kununua baada ya kuifungia Yanga bao la mapema dakika 24, kwa mpira wa adhabu uliokwenda moja kwa moja wavuni.

Mshambuliaji huyo Ajib aliwainua mashabiki wa Yanga dakika 30, kwa kuunganisha kwa shuti kali krosi ya chini ya Obrey Chirwa.

Mabao hayo yanamfanya Ajibu kufikisha magoli matano akiwa nyuma kwa mabao matatu kwa kinara wa ufungaji Emmanuel Okwi mwenye magoli nane baada ya kucheza mechi saba za Ligi Kuu Bara.

Mabao mengine ya Yanga yalifungwa na kiungo Pius Buswita katika dakika 54, kabla ya Mzambia Chirwa kuhitimisha kalamu hiyo kwa kupachika bao la nne.

Kipigo hicho kilimlazimisha kocha wa Stand United, kumtoa kipa Frank Muwonge nafasi yake kuchukuliwa na Mohamed Makaka katika dakika ya 71.

Bao la Ajib alilofunga dakika ya 24, limefanana na lile la Njombe Mji kupitia mpira wa adhabu, jambo lililozidi kumpatia umarufu zaidi ndani ya kikosi hicho anachochezea kwa msimu wa kwanza akitokea Simba.

Ajibu alitolewa nje dakika ya 71 nafasi yake ikachukuliwa na Juma Mussa, lakini bado Yanga, ilionyesha kucheza kwa kujiamini huku Stand United, ikionekana kuwa na presha ya juu.

Benchi la ufundi la Stand United, kadri dakika zilivyokuwa zinayoyoma lilionekana kukata tamaa zaidi huku wakiwa hawana la kufanya juu ya kipigo hicho cha mabao 4-0.

Yanga na Simba, zinakutana Oktoba 28, huku zikiwa na ari ya mchezo baada ya Wekundu wa Msimbazi kuibuka na ushindi wa mabao 4-0 dhidi ya Njombe Mji na Yanga ikiwafunga Stand 4-0.