Ajib, Banka waitibulia Yanga

YANGA inaendelea kupewa dozi nzito ya mazoezi hapa Bigwa milimani Mkoani Morogoro lakini kuna watu wawili tu wanapasua kichwa cha kocha wao Mwinyi Zahera.

Akizungumza na Mwanaspoti Kocha Mkuu wa Yanga, Mwinyi Zahera amesema mpaka jana alikuwa anawakosa kiungo Mohamed Issa ‘Banka’ ambaye bad hajajiunga na timu hiyo.

Zahera alisema Banka alikuwa na ruhusa maalum ya kushughulikia uhamisho wake wakati akitua Yanga msimu huu akitokea Mtibwa Sugar lakini bado ahataka kumuona mapema katika kikosi chake.

Kocha huyo raia wa DR Congo alisema endapo Banka ataendelea kuchelewa anaweza kupishana na sehemu kubwa ya mazoezi muhimu wanayoyafanya sasa.

Mbali na Banka Zahera amesema pia bado haelewi kwanini mshambuliaji wake Ibrahim Ajib hayupo katika kambi yao mpaka sasa.

Alisema alijulishwa kuwa Ajib ni mgonjwa wa maralia lakini hadhani mpaka sasa atakuwa hajapona anachoumwa kuweza kuungana na timu hiyo.

“Tunamkosa Banka unajua tangu asajiliwe hajajiunga aliniomba ruhusa nikamkubalia lakini hatakiwi kchelewa zaidi atakosa hii programu ni muhimu kwake,”alisema Zahera

“Mwingine ni Ajib,hayupo na sisi hapa niliambiwa anaumwa lakini sidhani kama mpaka sasa atakuwa hajapona sasa sijaelewa ana tatizo gani lingine uongozi watajua.”