Ah! Kumbe tatizo Simba, Yanga bwana

Muktasari:

Viingilio katika mchezo huo VIP A 30000, VIP B 20000, Viti vya machungea na Kijani 7000 na tiketi zitaanzwa kuuzwa mapema kuanzia Septemba 20.

Dar es Salaam. Kilio cha Ofisa Habari wa Simba, Haji Manara juu ya watani wao wa jadi Yanga kucheza mechi 11 mfululizo jijini Dar es Salaam kinatoa ishara ya hofu ya klabu yake kuelekea mechi baina ya timu hizo, Septemba 30 jijini.

Juzi Jumatano, Manara kupitia ukurasa wake wa Instagram alionyeshwa kushangazwa na ratiba ya Ligi kuipa nafasi Yanga ya kucheza mechi 11 mfululizo za Ligi Kuu jijini Dar es Salaam.

"Haijawahi kutokea kokote dunia toka Ulimwengu umeumbwa, klabu moja kucheza mechi 12 mfululizo kwenye kituo chake. Usisahau JKT, Simba, KMC na African Lyon zitachezewa Taifa. Hoja hapa ni nini?" alihoji Manara.

Michezo hiyo 11 mfululizo ambayo Yanga watacheza jijini ni dhidi ya timu za Stand United, Coastal Union, Singida United, JKT Tanzania, Simba, Mbao FC, Alliance, KMC, Lipuli, Ndanda  na African Lyon.

Ingawa Manara ameonekana kuzinyooshea kidole mechi 11 za Yanga zitakazochezwa hapa jijini, mchezo baina ya timu hizo mbili kongwe unaonesha dalili kuwa ndio chanzo cha malalamiko hayo tofauti na michezo mingine 10 iliyobakia.

Ratiba ya Ligi Kuu Tanzania Bara inaiweka katika wakati mgumu Simba kuelekea mchezo huo huku ikiwatengenezea mazingira mazuri watani wao Yanga kupata maandalizi mazuri kabla ya mechi baina yao.

Uamuzi wa Bodi ya Ligi Kuu kutobadili tarehe ya mchezo wa Watani wa Jadi kama ilivyotarajiwa, unaweza kupokelewa vyema na Yanga ambao ratiba ya Ligi inawapa nafasi ya kucheza mechi hiyo wakiwa wamepata muda wa kutosha kujiandaa kulinganisha na Simba.

Simba italazimika kufanya kazi ya ziada kujiandaa na mchezo huo kwani kabla ya hapo italazimika kusafiri umbali mrefu kwenda mikoani kucheza mechi tatu mfululizo kati ya minne kabla ya kukutana na Yanga tofauti na watani wao ambao wenyewe mechi zao zote kabla ya mechi hiyo watachezea hapa jijini.

Wakati Yanga ikibakia jijini kucheza na Stand United, Coastal Union, Singida United, JKT Tanzania kabla ya kuivaa Simba, watani wao watakuwa wanasafiri umbali wa zaidi ya Kilomita 2865 katika miji tofauti nchini ambako wataenda kucheza mechi zao za Ligi kabla ya kurejea jijini kuikabili Yanga.

Simba ambao wako Mtwara walikotua na ndege jana asubuhi kwa ajili ya mechi ya kesho dhidi ya Ndanda FC, baada ya mchezo huo watalazimika umbali wa Kilomita 1708 hadi Mwanza ambako watacheza na Mbao FC, Septemba 20 na baada ya hapo watasafiri umbali wa Kilomita 168 kutoka Mwanza hadi Shinyanga wakatakapoumana na wenyeji Mwadui FC, Septemba 22.

Baada ya hapo Simba italazimika kusafiri umbali wa Kilomita 1011 kutoka Mwadui hadi Dar es Salaam ambapo itakuwa na mchezo dhidi ya Biashara United, Septemba 27 na kisha itakuwa na siku mbili tu za maandalizi kabla ya kuvaana na Yanga.

Hata hivyo mambo yanaweza kugeuka mzunguko wa pili kwani Yanga watalazimika kutoka nje ya Dar es Salaam kwenye idadi kubwa ya mechi jambo linaloweza kuinufaisha Simba kinyume na ilivyo sasa ambapo wao ndio wanaonekana wanufaika zaidi.

Lakini katika hali ya kushangaza hata Simba wenyewe nao ni wanufaika wa ratiba kwani nao watacheza mechi nane mfululizo jijini mara baada ya kumaliza mechi zake za ugenini dhidi ya Ndanda, Mbao na Mwadui FC.

Ikishamalizana na Biashara United pamoja na Yanga, mechi nyingine sita mfululizo ambazo Simba watacheza hapa jijini ni dhidi ya African Lyon, Alliance, Ruvu Shooting, JKT Tanzania na KMC.

Akizungumzia suala la ratiba hiyo, Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Ligi, Boniface Wambura alisema haina tatizo lolote.

"Ukitazama utagundua kwamba mkoa wa Dar es Salaam pekee kuna timu kama tano ambazo zikicheza na Yanga au Simba zinatumia Uwanja wa Taifa au Uhuru ambazo ni African Lyon, Ruvu Shooting, JKT Tanzania na KMC.

“Kutokana na hilo, vyovyote ambavyo ratiba ingepangwa bado mechi hizo zingechezwa Dar es Salaam tu na ratiba imekuwa na uwiano mzuri kwa timu kucheza mechi za nyumbani na ugenini," alisema Wambura.

Ofisa Habari wa klabu ya Yanga, Dismas Ten alionyesha kushangazwa na wanaolalamika juu ya ratiba kuipendelea Yanga.

"Siyo mechi zote Yanga ndio tutakuwa wenyeji wa mchezo. Michezo mingine sisi tutakuwa ugenini na watu wanapaswa kukumbuka kuwa wanaopanga ratiba ni bodi ya ligi," alinukuliwa Ten.

Ofisa Habari wa TFF, Clifford Ndimbo alisema mchezo huo upo na utapigwa Septemba 30.

"Mchezo wa Simba dhidi ya Yanga upo na utachezwa siku iliyopangwa kama kawaida  na mashabiki wajitokeze kushabikia timu zao kwenye siku hiyo," alisema.

Ndimbo aliongeza kwamba katika mchezo huo wamezidisha ulinzi wa kutosha ili mashabiki waweze kuwa na amani muda wote wakiwa wanafatilia mchezo huo.

Viingilio katika mchezo huo VIP A 30000, VIP B 20000, Viti vya machungea na Kijani 7000 na tiketi zitaanzwa kuuzwa mapema kuanzia Septemba 20.