Timu vigogo Afrika Kusini zamuwinda Abdi Banda

Muktasari:

Miamba hiyo ya soka nchini humo ilikuwa inatajwa kuvutiwa na kiwango cha beki huyo wa Baroka ambaye tangu atue kwenye kikosi hicho amekuwa mchezaji muhimu kwenye safu ya ulinzi.

Dar es Salaam. Miamba ya soka nchini Afrika Kusini, Orlando Pirates, SuperSport United F.C na Kaizer Chiefs itawalazimu kusubiri mpaka mwishoni mwa msiumu wa 2017/2018 ili kupigana vikumbo kwa ajili ya kuinasa saini ya beki wa kimataifa wa Tanzania, Abdi Banda.
Miamba hiyo ya soka nchini humo ilikuwa inatajwa kuvutiwa na kiwango cha beki huyo wa Baroka ambaye tangu atue kwenye kikosi hicho amekuwa mchezaji muhimu kwenye safu ya ulinzi.
Banda ameichezea Baroka michezo 14 ya Ligi Kuu Afrika Kusini ‘PSL’,ndani ya michezo timu yake ambayo ipo nafasi ya 6 imeshinda mara 4, sare mara 7 huku wakipoteza michezo 4 hivyo wanajumla ya pointi 19 kwenye msimamo.
“Uwezekano wa kuondoka kipindi hiki ni mdogo kwa sababu ni ngumu wao kupata mbadala wangu kwa muda huu mchache, hilo wameniweka wazi. Nimeamua kujikita kwenye namna ya kuendelea kuisaidia timu yangu kwa sasa na sio hayo mambo ya usajili,” alisema Banda.