ARTHUR Melo

Muktasari:

Arthur ataanza kuitumikia Barcelona mwaka 2019 baada ya makubaliano rasmi baina ya klabu hizo. Mashabiki wengi wanataka kumjua zaidi staa huyu ambaye anafuata nyayo za wakongwe wengine wa Brazil waliokipiga Nou Camp.

SAO PAULO, BRAZIL

HATIMAYE Barcelona imefanikiwa kuinasa saini ya kiungo wa kimataifa wa Brazil, Arthur anayekipiga Gremio pia ya Hispania.

Arthur ataanza kuitumikia Barcelona mwaka 2019 baada ya makubaliano rasmi baina ya klabu hizo. Mashabiki wengi wanataka kumjua zaidi staa huyu ambaye anafuata nyayo za wakongwe wengine wa Brazil waliokipiga Nou Camp.

Akulia timu ya Ronaldinho

Jina lake kamili ni Arthur Henrique Ramos de Oliveira Melo lakini anajulikana zaidi kwa jina moja la Arthur. Alizaliwa Agosti 12, 1996 Goiania, Brazil na mpaka sasa ana umri wa miaka 21 tu.

Arthur alianza kucheza soka katika klabu ya mtaani kwao ya Goiás akiwa na umri wa miaka 12. Mwaka 2010 alionwa na Gremio katika michuano ya vijana. Gremio ndio klabu iliyomuibua staa wa zamani wa Brazil, Ronaldinho.

Januari 2015, kutokana na kiwango chake kizuri katika michuano ya vijana ya Jimbo la Sao Paulo, Arthur alipewa promosheni ya kutoka katika kikosi cha vijana kwenda katika timu ya wakubwa iliyokuwa inafundishwa na kocha maarufu wa Brazil, Luiz Felipe Scolari.

Bila ya kutazamia alipangwa katika mechi yake ya kwanza dhidi ya Aimore. Hata hivyo, alitolewa wakati wa mapumziko na nafasi yake kuchukuliwa na beki wa KIargentina, Matías Rodríguez na baada ya hapo hakucheza tena mechi ya kikosi cha wakubwa.

Mwaka 2016, Arthur alicheza mechi yake ya kwanza ya ligi dhidi ya Botafogo ikiwa ni mechi ya mwisho ya msimu huo. Walichapwa bao 1-0 nyumbani huku Arthur akiingia katika kipindi cha pili kuchukua nafasi ya Kaio.

Mwaka 2017, Arthur alikuwa mchezaji wa kudumu katika kikosi cha kwanza huku akionyesha makali yake katika mechi za Ligi Kuu pamoja na michuano ya Jimbo la Campeonato Gaúcho. Katika mechi yake ya kwanza ya klabu bingwa ya Amerika Kusini maarufu kama Copa Libertadores Arthur alicheza vizuri katika sare ya 1-1 dhidi ya Guarani.

Katika pambano hilo alitajwa kama mchezaji bora wa mechi huku akikamilisha pasi 40 ambazo zilikuwa ni asilimia 100 ya mafanikio. Kiwango chake kilisababisha afananishwe na viwango vya mastaa wawili wa Hispania, Andrés Iniesta na Thiago Alcântara.

Haikuishia hapo, kiwango chake kilizivutia klabu mbalimbali za Ulaya zikiwemo Chelsea, FC Barcelona na Atlético Madrid. Klabu hizo zilianza kutuma wawakilishi mbalimbali katika Bara la Amerika Kusini kwa ajili ya kumtazama kwa karibu. Mei mwaka jana alifunga bao lake la kwanza katika soka la kulipwa katika pambano la Kombe la Brazil dhidi ya Fluminense. Bao lake lilikuwa la kuongoza katika pambano hilo ambalo walishinda mabao 3-1.

Julai alifunga bao lake la kwanza la Ligi katika pambano dhidi ya Vitoria katika ushindi wa mabao 3-1. Bao lake lilikuwa la pili katika mechi hiyo.

Avaa jezi ya Barca kimakosa

Desemba mwaka jana, Arthur alileta utoto baada ya kujikuta akivaa jezi ya Barcelona akiwa na ndugu zake. Kitendo hicho kilileta utata mkubwa kwa Gremio kumshutumu mchezaji huyo kwa kukosa maadili. Ilikuwa ni katika siku ambayo Barcelona ilicheza na Celta Vigo.

Wakati Wakurugenzi wa Gremio walikuwa wanajua mchezaji huyo alikuwa anahuhudhuria mechi hiyo iliyochezwa Nou Camp, waliamini staa wao alikuwa amevuka mipaka. Hata hivyo, baadaye tukio hilo liliwasaidia Barcelona.

Ingawa Gremio ilifikiria kulalamika Fifa lakini ilipokea simu ya msamaha kutoka kwa Mkurugenzi wa Masuala ya Ufundi wa Barcelona, Robert Fernandez na klabu hiyo ililainika na kuamua kuacha kwenda kulalamika Fifa.

Inadaiwa simu hiyo pia ilisaidia kwa kiasi kikubwa kuimarisha uhusiano baina ya klabu hizo na ndio ilikuwa chanzo cha mazungumzo baina ya timu hizo katika dili la kuuziana staa huyo.

Atinga Barcelona rasmi

Machi 11, 2018, baada ya miezi kadhaa ya maongezi, Gremio ilifikia makubaliano na Barcelona kuwauzia staa huyo. Hata hivyo, Barcelona imepewa muda hadi Julai 2018 kumnunua mchezaji huyo na ikishindwa basi timu nyingine itaruhusiwa kumnunua.

Ada yake inatazamiwa kuigharimu Barcelona kiasi cha Euro 30 milioni huku ongezeko la ada hiyo kutokana na kiwango chake likitazamiwa kuwa Euro 9 milioni. Endapo Barcelona ikikamilisha dili hilo, Arthur anatazamiwa kuanza kukipiga Barcelona mwakani.

Atinga jezi ya Brazil

Arthur ameiwakilisha Timu ya Taifa ya Brazil katika chini ya umri wa miaka 17 na 20 na kufanya vizuri katika michezo kadhaa.

Alikuwa sehemu ya kikosi cha Brazil chini ya umri wa miaka 17 ambacho kilishiriki katika michuano ya Amerika Kusini chini ya umri huo mwaka 2013.

Septemba 15, 2017, Arthur aliitwa kwa mara ya kwanza katika kikosi cha wakubwa cha Brazil ambacho kilikuwa kinajiandaa kucheza mechi za kufuzu Kombe la Dunia 2018 litakalofanyika Urusi, dhidi ya Bolivia na Chile.