Mastaa wa Tanzania wanavyopigania soka lao ughaibuni

Muktasari:

  • Nchi nyingi za Ulaya kama vile Ufaransa, Hispania, Italia, Ujerumani na nyinginezo, ukiachilia mbali England ambayo dirisha lao la usajili lilifungwa Agosti 9, zenyewe ilikuwa Agosti 31.

Dar es Salaam. Upepo wa dirisha la usajili umepita na nyota kadhaa wa Kitanzania wanaocheza soka la kulipwa kwenye nchi mbalimbali kuanzia barani Afrika  hadi Ulaya  kwa kuhama kutoka  klabu moja na kwenda nyingine.

Nchi nyingi za Ulaya kama vile Ufaransa, Hispania, Italia, Ujerumani na nyinginezo, ukiachilia mbali England ambayo dirisha lao la usajili lilifungwa Agosti 9, zenyewe ilikuwa Agosti 31.

Kwa upande wa Afrika nchi nyingi zinatofautiana tarehe za kufunguliwa na kufungwa kwa usajili ikiwemo Misri ambao dirisha lao lilifunguliwa Juni 3 na kufungwa Agosti 2.

MCL Digital inakuletea nyota wa Kitanzania baada ya msimu uliopita kumalizika, walihama kutoka timu moja kwenda nyingine ama kwa ajili ya kusaka malisho bora na wengine kwa ajili ya kupandisha viwango.

Said Mhando

Kiungo mshambuliaji, Said Mhando, 21, amejiunga na Ascoli Calcio inayoshiriki Ligi Daraja la Kwanza  Italia ‘Serie B’, Agosti  16 akitokea FC Chiasso ambayo nayo ni ya Daraja la Kwanza nchini Uswisi.

Hata hivyo, akizungumza na Spoti Mikiki kutoka nchii Italia, alisema kuwa hakucheza sana na klabu yake imeamua kumpeka kwa mkopo katika klabu ya AC Cuneo inayoshiriki Ligi Daraja la ‘Serie C’ kwa kuwa walimwomba mchezaji huyo.

Orgeness Mollel

Winga Orgenes Mollel ambaye aliwahi kuichezea timu ya taifa ya vijana ya U-20, Ngorongoro Heroes miaka ya nyuma.

Mollel ambaye leo kesho anatamani kuitwa Taifa Stars, baada ya msimu uliopita kumalizika, amejiunga na Tirsense ya Ligi Daraja la Pili nchini Ureno akitokea Famalicão iliyokuwa Daraja la Kwanza kwa kusaini mkataba wa mwaka mmoja utakaomalizika Juni 30, 2019.

“Unajua soka lazima utumie maarifa zaidi, huku kuna ushindani sana, na si unajua sisi Watanzania hatuko masikioni mwa watu sana, sasa watu wanaweza kunishangaa, lakini nina akili yangu.

“Nimelenga kupata nafasi zaidi ya kucheza ndiyo maana nimeamua kuondoka Famalicao, nataka kuonyesha zaidi kipaji changu halafu nitokee huku,” anasema Mollel.

Rashid Udikaluka

Kiungo Rashid Udikaluka ambaye alikuwa akiichezea AKA WAC ya Austria kwenye Ligi za vijana wenye miaka 18`, amejiunga na Spittal ambapo atakuwa akipata nafasi ya kucheza Ligi daraja la tatu.

Mchezaji huyo ambaye anaweza kuitumikia Ngorongoro Heroes kwa mashindano ya U-20, alisema pia umri wake umesogea na ndio sababu kubwa ya yeye kuondoka katika eneo la miaka 19 na kuanza na Ligi Daraja la Tatu akiamini atapanda taratibu.

Adolf Bitegeko

Kiungo mkabaji Adolf Bitegeko aliyekuwa akilelewa kwenye kituo cha chuo cha Lassen nchini Marekani ambapo pia alikuwa akijipatia elimu ya darasani, amejiunga na KR Reykjavík ya Ligi Kuu Iceland.

Akizungumza na Spoti Mikiki kutoka nchini Iceland anasema kuwa kwa sasa anataka kucheza soka ya ushindani akiamini siku moja ataitwa katika kikosi cha Taifa Stars.

“Huku maisha ya soka si mabaya, jamaa wako sawasawa, na mwaka huu timu yao iliingia kwenye Fainali za Kombe la Dunia kule Russia, kwa kweli wako na mipango.

“Maisha ya huku ni mazuri, bado sijaanza kukutana na changamoto zozote maana kama ni lugha asilia kubwa wanazungumza Kiingereza na pia msimu haujaanza ule ushindani, ni jambo la kusubiri,” anasema Bitegeko.

MAINGIZO MAPYA NJE

Hassan Kessy, Nkana Red Devils

Beki wa kulia, Hassan Kessy aliyezivuruga Simba na Yanga. Baada ya kutoongezewa mkataba wa kuendelea kuwatumikia Yanga, alipata dili la kujiunga na Nkana Red Devils ya Zambia kwa kusaini mkataba wa miaka miwili.

Kessy tangu ajiunge na Nkana wiki chache zilizopita, ameingia moja kwa moja kwenye kikosi cha kwanza cha timu hiyo inayoshiriki Ligi Kuu Zambia.

Shaaban Idd Chilunda, Tenerife

Baada ya kuwa mfungaji bora wa Michuano ya Kombe la Kagame, Chilunda ambaye alikuwa akiichezea Azam FC, alipata nafasi ya kusajiliwa na CD Tenerife ya Hispania kwa mkataba wa mkopo wa miaka miwili.

Mshambuliaji huyo mara baada ya kutua Hispania alipata namba kwa kuichezea klabu yake hiyo mpya kwenye mchezo wa Ligi Daraja la Kwanza Hispania dhidi ya Gimnàstic Tarragona ambapo alichangia kupatikana kwa sare ya bao 1-1.

Elias Maguli, AS Kigali

Nyota wa zamani wa Simba, Elias Maguli amejiunga na AS Kigali ya Rwanda kwa kusaini mkataba wa miaka miwili japokuwa bado mambo hayajakuwa mazuri, kwa kuwa utaratibu wa wachezaji wa nje haujakaa sawa.

Endapo mambo yatakaa kwenye mstari, mshambuliaji huyo anatarajiwa kuondoka nchini mwezi ujao ili akaungane na wenzake  kuanza maandalizi ya msimu mpya wa Ligi Kuu nchini humo.

Himid Mao, Petrojet

Kiungo mkabaji, Himid Mao ‘Ninja’ amejiunga na Petrojet ya Misri kwa kusaini mkataba wa miaka miwili akitokea Azam FC,

Tangu ajiunge na timu hiyo ya Ligi Kuu nchini humo  amekuwa mchezaji muhimu kwenye kikosi cha kwanza cha timu hiyo inayoshiriki Ligi Kuu ya Misri.

Ameisaidia timu yake ambayo mpaka sasa iko nafasi ya saba ikiwa imetoka sare nne na kushinda mmoja na haijapoteza.