Aguero apiga hat trick City ikiua 6-1

Manchester, England. Mshambuliaji mahiri wa Argentina, Sergio Aguero ameifungia Manchester City mabao matatu ‘hat trick’ katika ushindi wa mabao 6-1 dhidi ya Huddersfield.

Hiyo imekuwa hat-trick ya kwanza ya katika Ligi Kuu England msimu huu wa 2018/19, mabao mengine ya City yakifungwa na Gabriel Jesus, David Silva na bao la kujifunga la Terence Kongolo, bao la kufutia machozi la Huddersfield lilifungwa na John Stankovic.

Aguero anakuwa mchezaji wa pili katika Ligi Kuu England kufunga hat trick ya tisa akimkaribia shujaa wa New Castle United, Alan Shearer aliyefunga hat trick 11, kwa muda wote wa uchezaji wake.

Mara baada ya kufunga bao la tano ambalo lilikuwa la tatu kwa Sergio Aguero, mfungaji bora wa muda wote wa City, alipumzishwa zikiwa zimesalia dakika tisa.

Ushindi huo umeirudisha City kileleni mwa Ligi Kuu, ikifikisha pointi sita na mabao manane ya kufunga na bao moja la kufungwa, ikiishusha Chelsea ambayo pia ina pointi sita lakini ikizidiwa mabao ya kufunga.

Katika mchezo mwingine wa Ligi hiyo, Burnley ikiwa nyumbani ilifungwa mabao 3-1 na Watford. Wakati mchezo utakaochezwa baadaye usiku wa leo utawakutanisha Brighton itakayoikaribisha Manchester United.