Kocha wa Rwanda alia timu isivunjwe

Dares Salaam. Baada ya kufanikiwa kuifunga timu ya Taifa ya vijana chini ya miaka 17 ya Burundi, Kocha Mkuu wa Rwanda, Rwasamanzi Yves, amewaomba viongozi wa soka wasivunje timu hiyo.
Kocha huyo alisema kwamba umekuwa utamaduni kwa nchi nyingi za kiafrika kuzivunja timu baada ya kumalizika kwa mashindano. “Tunakuwa tunaziona hizi timu pale ambapo kunakuwa na Mashindano tu, lakini mpira unahitaji utaratibu mzuri ili kufikia malengo na vijana wanatakiwa watengenezwe vizuri,” alisema.
Akizungumzia mchezo wao dhidi ya timu ya Taifa ya Tanzania ‘Serengeti Boys’, alisema anatambua ugumu wa mchezo huo, lakini atajitahidi kupambana nao.
“Tanzania ni timu nzuri na hilo kila mmoja analijua, walicheza mpira mzuri dhidi ya Burundi ni ngumu kuzungumzia kabisa mchezo huu lakini tutajitahidi kupata matokeo,” alisema.
Naye kocha Bahati Vivier wa Burundi, alisema kupoteza dhidi ya Rwanda ilitokana na jinsi ambavyo safu yake ya ulinzi iliyumba na kuruhusu mabao ya mapema. (Thomas Ng’itu).