Timu za Yanga, Mkamba Rangers kuonyeshana ubabe

Dar es Salaam. Timu ya Daraja la Pili ya Mkamba Rangers ya Kilomero, leo inacheza mechi ya kirafiki na Yanga, mchezo ambao umepangwa kufanyika kwenye Uwanja wa CCM, Mkamba.
Mchezo huo ni sehemu ya maandalizi kwa timu zote mbili, huku Yanga ikiajiandaa na mechi za Ligi Kuu ya Tanzania Bara na mchezo wa kombe la Shirikisho dhidi ya timu ya USM Alger ya Algeria ambao utafanyika Agosti 19 kwenye uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Mmoja wa viongozi wa Mkamba Rangers, Juma Ligonela alisema kuwa walizungumza na uongozi wa Yanga kuhusiana na mchezo huo na kukubaliana.
Alisema kuwa mchezo huo pia utakuwa fursa kwa timu yao kuwapima wachezaji wapya na kuwaona wachezaji nyota wa yanga ambao wamejiunga msimu huu.
“Tumejiandaa vyema kwa ajili ya mchezo huo na utakuwa wa pili kucheza na timu za Ligi Kuu ya Tanzania Bara, mchezo wa kwanza tulicheza na Mbeya City, pia tulipata matokeo mazuri kwenye timu za madaraja ya chini,” alisema Ligonela.
Kocha wa Mkamba Rangers, Juma Omary Mpoka alisema kuwa watatumia fursa hiyo kukitambulisha kikosi chao na wachezaji wapya ambao wamewasajiliwa msimu huu.
Alisema kuwa wamesajili wachezaji wengi chipukizi na wenye vipaji  hivyo Yanga itegemee kupata upinzani mkali.