Yanga kuifuata Simba Arusha

Arusha. Wanachama wa klabu ya Yanga mjini Arusha walikutana mwishoni mwa wiki kujadili mambo kadhaa, wamekubaliana kuialika timu yao ili kupata fursa ya kumpa heshima ya kumuaga, Nadir Haroub ‘Cannavaro’ aliyestaafu soka na kuwa meneja mpya wa timu hiyo.
Makamu Mwenyekiti wa Yanga mkoani hapa, Mhina Kahoya alisema wanatambua mchango alioutoa Cannavaro wakati akiwa nahodha na mlinzi tegemeo wa kikosi hicho.
Alisema mlinzi huyo alikuwa kiungo cha mawasiliano kati ya viongozi wa Yanga na wachezaji, hivyo wameona bora waiite timu ya Yanga ikacheze mchezo wa kirafiki ambao utatumika kumuaga rasmi mkongwe huyo.
“Tutaialika Yanga ije Arusha ili tupate nafasi ya kumuaga Cannavaro, miaka ya nyuma viongozi wa Yanga, walikuwa na ushirikino mkubwa sana kwa matawi ya mikoani, lakini hapa katikati kuna watu wachahe waliharibu utamaduni huu, ndio maana tulikaa pembeni, ila kwa sasa tumerejea kuisapoti timu yetu,” alisema Kahoya.
Aliongeza kuwa kama watakubaliwa watautumia mchezo huo kama moja ya njia ya kukabidhi michango yao kwenye timu na hata kama wakikosa basi kuna njia nyingi wataitumia kukabidhi michango watakayokusanya kwa uongozi. “Hapo awali Arusha ilikuwa inahusika hadi kwenye usajili wa timu, viongozi wa makao makuu wakisema kocha anamtaka mchezaji wa nafasi fulani, sisi tulikuwa tunatoa fedha za kuhakikisha mchezaji anapatikana.”
Sambamba na hayo, Kahoya alisema wamekubaliana kuanza mchakato wa uchaguzi wa tawi kabla ya kumalizika mwaka huu, pamoja na kuongeza wanachama wengine wapya kutoka mkoani Arusha.
Mchezo wa Yanga na Mawenzi Market uliofanyika kwenye Uwanja wa Jamhuri, Morogoro, vijana hao wa Jangwani waliibuka na ushindi wa bao 1-0.

Simba ipo mkoani Arusha ambako inacheza mchezo wake wa kirafiki dhidi ya Arusha United ikiwa ni maandalizi ya msimu mpya wa Ligi Kuu Bara.