Bakayoko atimkia AC Milan

London, England. Kiungo wa Chelsea, Tiemoue Bakayoko amejiunga na miamba ya Italia, AC Milan kwa mkataba wa mkopo wa muda mrefu.

Kiungo huyo mwenye miaka 23, ambaye ameichezea Ufaransa mechi moja 2017, aliweza kucheza mechi 43 katika kikosi cha Chelsea huku akianza katika michezo 34.

Lakini hayupo katika mipango ya kocha Maurizio Sarri na katika mchezo wa kwanza wa Ligi Kuu Chelsea waliposhinda 3-0 dhidi ya Huddersfield Jumamosi iliyopita.

Bakayoko alijiunga na Chelsea akitokea Monaco Julai 2017 kwa mkataba wenye thamani ya pauni 40milioni.

Msimu huu Chelsea imeongeza kiungo Jorginho aliyetoka timu aliyokuwa akifundisha Sarri ya Napoli kwa gharama ya pauni45milioni pamoja na Mateo Kovacic aliyesajiliwa kwa mkopo kutoka Real Madrid.

Pia, nyota wa England, Ruben Loftus-Cheek amerudishwa akitokea Crystal Palace alipokuwa kwa mkopo.

Jorginho, N'Golo Kante na Ross Barkley walianza katika kikosi cha Chelsea Jumamosi huku Loftus-Cheek akiingia kuchukua nafasi ya Barkley katika dakika 68.