AUSSEMS: Akiuchezea ule mziki wa Jangwani, inakula kwake mapema tu Simba

Kocha Mkuu Mpya wa Simba, Patrick Aussems kutoka Ubelgiji.

MWANDISHI WETU. SIMBA imeanza maisha mapya ikiwa na Kocha Mkuu Mpya, Patrick Aussems kutoka Ubelgiji. Kocha Aussems ndio kwanza anaingia wiki ya tatu tangu asaini mkataba wa mwaka mmoja wa kukinoa kikosi hicho cha mabingwa wa soka nchini.

Wiki mbili za awali alikuwa kambini na timu hiyo wakijiandaa na mechi za msimu mpya. Kambi ilikuwa Uturuki na kikosi chake kilicheza mechi mbili kabla ya kurejea nchini mapema wiki hii na kucheza mechi ya Simba Day dhidi ya Asante Kotoko.

Achana na sare ya 1-1 iliyopata na Waghana, Kocha huyo wa zamani wa AC Leopards ya Kongo ametua Msimbazi, timu ikitoka kubeba taji la kwanza la Ligi Kuu tangu mwaka 2012. Simba ilibeba taji hilo chini ya mikono ya makocha Joseph Omog, Djuma Masoud na mwishowe, Mfaransa Pierre Lechantre. Omog na Lechantre

tayari wameshaondoka kikosini.

Omog alisitishiwa mkataba wake baada ya matokeo ya mechi ya Kombe la FA, Simba ilipovuliwa taji na Green Warriors.

Lechentre hakuongezewa mkataba kwa madai ya kuwa na gharama kubwa na klabu haikumudu ndipo akaletwa Aussems.

Hata hivyo, inawezekana kabisa Aussems ameshadokezwa juu ya ishu za Yanga na Simba katika soka la Tanzania, lakini Mwanaspoti linatoa mwongozo tu kwa Mbelgiji huyo kama anataka mambo yamnyooke Msimbazi.

TUMAINI JIPYA

Baada ya Omog na Lechantre kuiondolea Simba unyonge, Aussems kwa sasa ni tumaini jipya la kuirejeshea Simba heshima iliyokuwa nayo miaka kadhaa nyuma, hasa anga za kimataifa.

Kwa namna rekodi za kocha huyo zinavyoonyesha ni wazi, Simba kama itaishi naye vizuri anaweza kuifanya timu hiyo kuwa tishio.

Aussems ataifikisha Simba mbali na kurejesha furaha Msimbazi baada ya mateso ya muda mrefu.

Bahati nzuri ni watani zao waliowatambia kwa misimu kadhaa na kuwabatiza majina mabaya kwa sasa hawapo vizuri.

AJICHUNGE HAPA

Hata hivyo, kuna jambo ambalo Kocha Aussemsanapaswa kuliepuka ili mambo yake yamnyooke Msimbazi. Asijaribu kuiwaza sana Yanga. Itampasua kichwa.

Ni kweli Yanga ni wapinzani na watani wa jadi ya Simba. Kwa sasa watani zao wapo hoi baada ya kuwa na mafanikio kwa misimu kadhaa mfululizo iliyopita. Ni kiu ya wadau wa Msimbazi kuona wanazima tambo za wapinzani wao hao. Na hilo linaweza kuwa kipimo cha kwanza kwa Kocha Aussems kuona anafanikiwa ama

kufeli Msimbazi kupitia pambano la watani.

Simba na Yanga ndivyo zilivyo. Sio mbaya kuweka mikakati ya kuizima Yanga, lakini nilidhani Aussems asielekeze nguvu nyingi huko na kusahau mechi nyingine.

Kuifunga Yanga katika mechi mbili zitaipa timu yake pointi sita tu, lakini katika mechi nyingine 36 za msimu ujao zinazoweza kumzalishia pointi 108.

Hivyo ni lazima ikomalie mechi hizo avune pointi nyingi kuliko kuwawaza watani.

Bahati nzuri alishakaririwa kwamba anajua kama wapinzani wakubwa wa Simba ni Yanga, lakini ajue matokeo yoyote mabaya katika mechi ya watani ni mkosi kwake,

lakini kupoteza ubingwa kunaweza kuwa balaa zaidi kwa Mbelgiji huyo.

ITAKULA KWAKE

Kama Aussems ametua Simba kwa akili ya kuhakikisha anaiwezesha Simba kuifunga Yanga tu, basi ajiandae kufungashiwa virago mapema hata kabla mwaka wake wa mkataba wake Msimbazi haujakamilisha.

Hii ni kama atapata matokeo mabaya katika mechi nyingine hata zile za mabonanza. Simba ndivyo walivyo!

Kocha Aussems aangalie tu rekodi za makocha wenzake waliomtangulia Simba walidumu Msimbazi kwa muda gani. Asiende mbali amtazame Dylan Kerr alivyoondoshwa kwa matokeo ya Kombe la Mapinduzi tu, kisha akampisha Omog.

Pia amuangalie Omog aliyeondoshwa akiiacha Simba kileleni mwa msimamo katika Ligi Kuu Bara, lakini matokeo ya Kombe la FA dhidi ya timu ya Daraja la Pili (SDL) ikamponza na kufurushwa kama mkora fulani tu!

MUHIMU ZAIDI

Sina maana ya kutaka Kocha Aussems akae Msimbazi kwa tahadhari kubwa, ila rai yangu kwake ni kuona anaibadilisha Simba iwe timu ya kupambana bila kuchoka.

Timu yenye wachezaji wenye kiu ya kuifikisha mbali timu yao, wasiridhike na matokeo ya mechi moja ama mbili tu, ligi ni ngumu, pia kuna michuano ya Kombe la FA linalotoa nafasi ya uwakilishi wa nje, nako isizembee.

Pia kuna Ligi ya Mabingwa ya Afrika ambayo anatakiwa kuhakikisha Simba inafika mbali na kuthibitisha kuwa kweli wao ndio Wazee wa Kimataifa kuanzia Desemba mwaka huu.

Ila muhimu zaidi ni kwa mabosi wa Simba sambamba na wanachama, mashabiki na hata wachezaji kuwa, wampe nafasi Aussems na kumpa ushirikiano wa kutosha ili afanye kazi na kukijenga kikosi ikizingatiwa ni kama kimeundwa upya kutokana na ingizo jipya la nyota kadhaa.

Naamini inahitajika muda wa wachezaji kuzoeana na kocha wao kabla ya kuanza kufanya yao ili kuwapa furaha Wanamsimbazi wote.