Pele anasema hivi Liverpool mabingwa

LIVERPOOL, ENGLAND
GWIJI la soka la Brazil, Pele ametoa utabiri wake na kusema kipa Alisson Becker na mshambuliaji Roberto Firmino ambao wote ni Wabrazili wataisaidia Liverpool kubeba ubingwa wa Ligi Kuu England msimu huu.
Liverpool ilimaliza kwenye nafasi ya nne katika msimu uliopita ambapo Manchester City walibeba ubingwa, lakini Pele anaamini kwamba safari hii wakali hao wa Anfield watamtoa kapa Pep Guardiola na chama lake la huko Etihad.
Pele anaamini kuwasili kwa kipa wa Kibrazili kwenye kikosi cha Liverpool, Alisson na kuwapo kwa mshambuliaji kiraka Firmino kutamfanya kocha Jurgen Klopp kuwa na wachezaji wenye uwezo wa kumpatia matokeo mazuri ndani ya uwanja.
Kubeba ubingwa ni mtihani mzito kwa Liverpool kwani tangu iitwe Ligi Kuu England hawajawahi kufanya hivyo, huku kushika nafasi ya pili tu, wamefanya hivyo mara mbili ndani ya miaka 10 iliyopita. Ubingwa wao wa mwisho wa ligi walibeba mwaka 1990.
Wababe hao wa Anfield leo Jumapili watashuka uwanjani kumenyana na West Ham United kwenye mchezo wao wa kwanza wa Ligi Kuu England.