HAACHWI MTU: Mademu waliohama na waume zao dirisha hili

LONDON, ENGLAND. UTAMU wa dirisha la usajili huwa unaleta raha kweli kweli. Unajua nini, kinachotokea si kuhamishwa kwa wachezaji tu, bali warembo wa wachezaji hao ambao wamekuwa wakiandamana na waume zao kila wanapokwenda jambo linalowafanya timu zinazowasajili kuongeza mvuto kwenye majukwaani ya viwanja vyao vya nyumbani.

Hawa hapa mademu bomba watano ambao wamehusika kwenye usajili wa majira ya kiangazi ya mwaka huu ambao watakwenda kuleta utamu na mvuto mpya kwenye timu walizokwenda kujiunga nazo.

5.Tiziri Digne (Lucas Digne)

Lucas Digne alisema kwamba anataka kuonyesha kiwango chake bora kabisa cha soka huko Everton baada ya kukamilisha uhamisho wake wa Pauni 18 milioni akitokea Barcelona. Digne alisema huwa haogopi kufanya mambo yake bora kabisa ndani ya uwanja, lakini jambo hilo pengine linachochewa zaidi kutokana na kuwapo kwa mrembo matata kabisa, Tiziri Digne. Mrembo, Tiziri yuko vizuri kweli kweli na hakika Everton wameongeza shabiki mwingine mrembo kwenye majukwaa yao ya uwanja wa Goodison Park. Tiziri ni maarufu kweli kweli, huko kwenye Instagram ana wafuasi 51,000.

4.Georgina Rodriguez (Cristiano Ronaldo)

Cristiano Ronaldo karuka wee, lakini kwa mrembo Georgina Rodriguez ndiyo mwisho wa reli. Kwa sasa supastaa huyo mpya wa Juventus hapindui kwa mrembo huyo na kinachosubiriwa kwa sasa ni ndoa tu baada ya kufanikiwa kupata mtoto mmoja wa kike. Uhamisho wa Ronaldo kutoka Real Madrid kwenda Juventus utamhusisha pia mrembo Georgina kwa sababu ni mtu anayefuatana naye kila anapokwenda, kampani yake hata kwenye sherehe. Hivyo, mashabiki wa Serie A watakuwa wamepata shabiki mpya kwenye mechi zao ambazo watamwona kwenye jukwaa la mechi za mabingwa hao wa Italia.

3.Anna Sharypova (Andre Schurrle)

Baada ya miaka mitatu, staa wa Kijerumani, Andre Schurrle amerejea tena kwenye soka la England, lakini safari hii ametua kwenye kikosi cha Fulham, licha ya kwamba ipo kwenye jiji lilile la London, ambalo huko nyuma aliwahi kuishi alipokuwa kwenye kikosi cha Chelsea. Lakini, ujio wa sasa wa staa huyo utamhusisha na mpenzi wake mrembo kabisa, Anna Sharypova, ambaye atakuwa akipambana uwanja wa Fulham kwenye mechi za Ligi Kuu England. Anna ni mrembo maarufu sana kwenye mitandao ya kijamii, akiwa na wafuasi kibao.

2.Izabel Kovacic (Mateo Kovacic)

Kiungo wa Croatia, Mateo Kovacic amehama kutoka Real Madrid na kutua Chelsea. Jambo hilo limemfanya kubadili ligi kutoka kwenye La Liga na kutua Ligi Kuu England. Lakini, kwenye safari yake hiyo ya London, ameongozana na mrembo kweli kweli, Izabel. Ile paap, umekutana na Izabel, usipokuwa makini utasema umekutana na Shakira, kwa sababu wanafanana kwa kiwango fulani. Hivyo, kwa mashabiki wa Stamford Bridge msimu huu watashangilia na mrembo anayefanana kabisa na Shakira. Usajili mzuri.

1.Natalia Loewe (Alisson Becker)

Mbrazili, Alisson Becker amekuwa kipa ghali namba mbili duniani baada ya kukamilisha uhamisho wake uliogharimu Pauni 67 milioni kutoka AS Roma kwenda Liverpool. Lakini, kuhama kwa Mbrazili huyo kumemhusisha pia mrembo mmoja matata sana, Natalia Loewe, ambaye ameungana na kipenzi chake kuhama Roma na kwenda Liverpool. Kwa maana hiyo, Liverpool wamepokea shabiki mwingine matata kabisa atakayekwenda kupamba majukwaa yao huko Anfield.