Guardiola atamani kula kichwa cha mtu

MANCHESTER, ENGLAND. KOCHA Mkuu wa Manchester City, Pep Guardiola amekasirishwa na madai yanayotolewa na chama cha soka cha Argentina kuhusu yeye.
Rais wa Chama cha soka cha Argentina (AFA), Claudio Tapia alisema kwamba walijaribu kumfuata Guardiola baada ya kumfuta kazi kocha Jorge Sampaoli, lakini walichokutana nacho ikiwa ni matakwa ya Mhispaniola huyo yamewakatisha tamaa.
Guardiola aliamua kulijibu hilo juzi Ijumaa, akisema: "Nimehuzunika sana kwa sababu rais wa chama cha cha soka Argentina hakupaswa kusema kwamba imeshindikana kunifikia mimi kwa sababu ya mshahara wangu.
"Kutokana na hilo, kwanza anapaswa kufahamu mshahara wangu na pia anapaswa kufahamu ninanchotaka kwa sababu kuifundisha timu ya taifa ni tofauti na klabu na kitu cha tatu, hakuna aliyewasiliana na mimi.
"Nina mkataba na Manchester City na nataka kuufanyia kazi, lakini mjadala wa kuhusu mshahara wangu hauna maana.
"Timu ya Argentina inapaswa kunolewa na Muargentina, kuna makocha wazuri sana wa Kiargentina wapo, mimi siwezi kwenda kuwa kocha wa Argentina. Sijui nini kitatokea huko baadaye, lakini usiseme kwamba hatumfuati Pep kwa sababu ya mshahara wake."