Polisi waliohusika kumpiga Mbise Uwanja wa Taifa wachukuliwe hatua

Mwanahabari Silas Mbise

INASIKITISHA, inaumiza na kutia simanzi kuona baadhi ya askari polisi wakishindwa kufanya kazi zao kwa weledi na umakini na badala yake kuishia kutumia nguvu bila sababu.

Kitendo kilichofanywa na baadhi ya askari waliokuwa zamu kwenye Tamasha la Simba Day, cha kuamua kumshambulia kwa kipigo kikali kama wanayeua paka mwizi, mwanahabari Silas Mbise kimetusikitisha na tunakilaani na kukikemea kwa nguvu.

Inatia aibu kwa askari aliyeenda na kuhitimu mafunzo chuoni kushindwa kujua ni eneo gani na kwa mtu gani anayepaswa kutumia nguvu kubwa kumdhibiti raia asiyekuwa na silaha wala hatia.

Kitendo hicho cha kumshambulia kwa kipigo mwanahabari huyo, hakikubaliki, pia kinaonyesha wazi jinsi Watanzania tusivyo salama mbele ya walinda usalama wetu.

Tunalisema hili kwa kurejea matukio mengi ya utumiaji wa nguvu na vishindo pasi na sababu kwa raia wasio na silaha wala kuwa na ukorofi.

Polisi wamekuwa wakitumia nguvu kubwa na wakati mwingine kutumia silaha za moto na kufyatua mabomu ya machozi bila sababu katika matukio yanayohitaji hekima na busara tu kutuliza raia.

Inawezekana haya wanayafanya kwa kutambua raia na wale wanaowaumiza hawana wa kuwatetea wala kuwalinda kama wanavyolindwa wao na wakubwa zao.

Mwanaspoti tunayasema haya kwa uchungu kutokana na ukweli matukio ya unyanyasaji kwa Wanahabari wanapokuwa wakitekeleza majukumu yao ni mengi na yanazidi kukithiri, huku kukiwa na ukimya katika kukemea na kuyalaani haya.

Achana na matukio ya kuuawa kwa Daud Mwangosi ama kupigwa na kujeruhiwa kwa Christopher Kidanka katika lile sakata la Ukonga, wanahabari wa michezo wamekuwa waathirika wa mikong’oto ya askari polisi. Unyanyasaji huu mpaka lini?!

Kilichompata Mbise na sehemu ya unyama unaofanywa na askari katika maeneo ya michezoni dhidi ya wanahabari na hata raia wa kawaida, lakini hakuna hatua zinazochukuliwa. Tumekuwa tukishuhudia mara kadhaa askari polisi kutumia mabomu ya machozi katika viwanja bila kujali wanaoenda uwanjani wapo watoto, wagonjwa hasa wa pumu na watu wenye ulemavu.

Tuliona kwenye vurugu za mechi ya Simba na Yanga ya Oktoba 1, 2016 jinsi askari hao walivyotuliza fujo zilizosababishwa na mashabiki wa Simba. Tukio lile lilileta taharuki kubwa kwa waliokuwa uwanjani hapo.

Nasi kama chombo cha habari tulipiga kelele na kulaani kama tunavyolaani sasa na tungependa wahusika na tukio la Mbise wachukuliwe hatua kali za kisheria.

Kuyanyamazia matendo hayo yanayofanywa na askari hao wachache wasio na uadilifu, huruma wala utu dhidi ya Watanzania wenzao na kijana mdogo kama Mbise ni kulea ugonjwa na kufanya askari wengine kufanya makosa kama hayo.

Hata kama Mbise alipotoka katika mzozo dhidi ya askari wakati wanahabari wanazuiwa kuingia chumba cha mikutano pale Taifa, bado kwa mafunzo waliyonayo askari hao wangeweza kumdhibiti na kumfikisha katika mikono stahili badala ya kile walichomfanyia, kumvua shati. Askari hayuko juu ya sheria, anatakiwa kusimamia sheria na haki.

Kiutaratibu ni kwamba, kama muhusika amekaidi amri na kuhatarisha usalama wa eneo husika, polisi wanalazimika kutumia nguvu, lakini si kwa mwanahabari huyu.

Hivi wao wanaamini walichomfanyia Mbise alistahili kwa kupigwa kama Jambazi? Hii ni aibu na kwa kuwa yapo matukio mengi ya aibu ambayo yamekuwa yakifanywa na polisi dhidi ya raia wema, ifike wakati yaishe.

Tunaamini Mkuu wa Jeshi la Polisi, IGP Simon Sirro ni mtu makini, muadilifu na anayeongozwa na busara, ni wazi atachukua hatua kwa wote waliohusika kumsulubu Mbise. Kadhalika kwa nafasi yake atumie kuwaelimisha zaidi askari polisi kuwa, matendo yao ya ovyo yanasababisha raia kupoteza imani na jeshi lao na pia wanalitia aibu bila sababu ya maana.

Matendo ya kuwanyanyasa raia wema na watu wasio na silaha ni kuonyesha kukosa hekima, weledi wa kazi na pengine wameingia kimakosa katika jeshi hilo na wanastahili kutolewa. Askari polisi ni lazima wawe rafiki na wema kwa raia kwa kuwa wao ndio walinzi wa usalama wa raia na mali zao na sio wasulubishaji!

Haipaswi kufikia hatua raia kumchukia polisi na kumwona kama adui kwa sababu ya matendo ya askari wachache wasio na uadilifu na uaminifu. Tunakataa, pia tunarudia kulaani uhuni aliofanyiwa Mbise, tukiwakumbusha askari polisi kuwa, wao ni tegemeo la taifa na Watanzania. Wabadilike na kama upolisi hawauwezi, watafute kazi nyingine za kufanya, sio lazima wawe askari.