ARSENAL YA LEO HII HAPA

LONDON, ENGLAND. SI unajua Jumapili ya leo kuna kile kipute matata huko Emirates kati ya Arsenal na Manchester City kwenye Ligi Kuu England, basi bana kocha Unai Emery ameshafahamu atatokajetokaje kwenye mechi hiyo.
Kocha huyo mpya huko Arsenal, Emery ambaye ameanza ujanja ujanja kwa kusema kwamba Pep Guardiola ni bora kuliko yeye, ataingia uwanjani na fomesheni ya 4-2-3-1.
Hata hivyo, kama utakuwa umemkariri Emery kwa fomesheni hiyo pekee, basi itakula kwako, kwani kikosi chake kitabadilika kwa kadri mechi inayokwenda na wakati mwingine ndani ya uwanja wataonekana wakiwa kwenye mtindo wa 4-3-3.
Kikosi ambacho kinatajwa kwamba kinaweza kuanzishwa kwenye kuwavaa mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu England, Man City, golini kutakuwa na mabadiliko makubwa, ambapo kipa mpya Bernd Leno ataanza mbele ya Petr Cech, huku kwenye safu ya mabeki kukitarajiwa kuwapo na Hector Bellerin, Sokratis Papastathopoulos, Shkodran Mustafi na Ainsley Maitland-Niles.
Kwenye safu ya kiungo, kutakuwa na Lucas Torreira, Granit Xhaka na Aaron Ramsey, huku kwenye fowadi kutakuwa na wakati Mesut Ozil, Henrikh Mkhitaryan na Pierre-Emerick Aubameyang.
Ligi Kuu England iliyoanza juzi Ijumaa, itaendelea leo kwa mechi kadhaa, ambapo Man City wataanzia ugenini kwa Arsenal, wakati Liverpool watakuwa nyumbani Anfield kucheza na West Ham United na Southampton watakipiga na Burnley.