Mourinho: Top Four tumwachie Mungu tu

London, England. Kocha Jose Mourinho ameumia baada ya wammiliki wa Manchester United, kutompa fedha za usajili, kwa hasira amesema hana uhakika kama atamaliza ndani ya nne bora ‘top four’.
Mourinho alibainisha hasira zake wakati akielezea maandalizi yake kuhusiana na mechi yao ya kwanza ya Ligi Kuu England itakayochezwa leo usiku dhidi Leicester City.
Alisema baada ya kushindwa kusajili kwa sasa anajipanga kuwatumia wachezaji waliopo kusaka pointi katika mchezo huo utakaofanyika kwenye uwanja wa Old Trafford.
Mourinho alisema kwa kutosajili kunampa wakati mgumu na sasa hana uhakika kama ataweza kuchuana na mahasimu wao Man City katika mbio za ubingwa kama ilivyokuwa msimu uliopita.
Alisema nia yake ilikuwa kukiboresha kikosi kilichomaliza Ligi kikipitwa pointi 19 na City, lakini hajui itakuwaje msimu huu.
"Nimelazimika kuweka mikakati kwa wachezaji hawa nilionao ila kwa hakika siamini kama tunaweza kumaliza katika nafasi ya pili tena,” alisema.
Kocha huyo alisema anajua ushindani umeongezeka City imejiimarisha, timu zilizomaliza katika nafasi za katikati zimesajili vizuri na zile zilizokuwa zikipigania kutoshuka zimejiimarisha pia hivyo ushindani sio wa kawaida.
Mourinho, anaianza Ligi bila wachezaji wake muhimu walioanza mazoezi siku chache zilizopita wakitokea mapumziko walioyapata baada ya kumalizika fainali za Kombe la Dunia 2018.
Wachezaji hao ni pamoja na kiungo Nemanja Matic, Antonio Valencia, Ander Herrera, na Marcos Rojo waliokosa mechi za maandalizi katika ziara ya Marekani.