Hakimu atoa siku saba Hanspoppe aondolewe kesi ya kina Aveva

Dar es Salaam.  Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu imetoa siku saba kwa upande wa mashtaka  kukamilisha mchakato wa kubadilisha hati ya mashtaka kwa kuwaondoa Zacharia Hanspoppe  na Franklin Lauwo ili kesi iweze kuendelea kwa Evans Aveva na Godfrey Nyange.

Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba akitoa siku hizo saba kwa upande wa mashtaka baada ya wakili wa Takukuru, Leonard Swai kueleza kesi ilipangwa kwa ajili ya kutajwa na washtakiwa Aveva na Nyange wapo mahakamani.

Swai leo Agosti 10, alidai kuwa mara ya mwisho mahakama ilitoa oda ya kuwaondoa Poppe na Lauwo katika hati ya mashtaka ili kesi iweze kuendelea kwa Aveva na Nyange.

"Utaratibu umefanyika na jalada tumepeleka kwa Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), nimejitahidi kufuatilia hadi leo asubuhi nimetoka kwa DPP, lakini hajaweza kulishughulikia kwa kuwa yupo nje ya Dar es Salaam, hivyo tunaomba tupewe wiki mbili kuhakikisha DPP analifanyia kazi hata kama atakuwa Dodoma tutamfuata huko huko ama Dar es Salaam." Alieleza Swai.

Baada ya Swai kueleza hayo, Aveva aliomba wapewe muda wa siku saba kwa sababu siku 14 ni nyingi na kuongeza kuwa upande wa mashtaka wanavyochelewesha jambo hilo wanawaumiza.

Nyange aliongeza kuwa jambo hilo la kubadilisha hati ya mashtaka kwa kuwaondoa washtakiwa hao ni la muda wa zaidi ya miezi miwili wakati wanajua wapo mahabusu kwa zaidi ya mwaka mmoja na kuendelea kukaa huko ni tatizo.

Alisisitiza  kuwa kuendelea kuwapatia upande wa mashtaka wiki mbili ni kama kuendelea kuwaficha Keko bila sababu za msingi.

Baada ya washtakiwa kulalamika hayo, Hakimu Simba alimuuliza Wakili Swai unaona malalamiko ya washtakiwa hayana msingi.

Swai alimjibu Hakimu Simba kuwa malalamiko yao yanamsingi mheshimiwa.

Hakimu Simba unasemaje na afya ya mshtakiwa wa kwanza Aveva inaonekana ana kliniki kila wiki nawapa siku saba mkamilishe taratibu, nyinyi upande wa mashtaka ndiyo mnachelewesha kesi kama hamuitaki simuifute na ameiahirisha hadi Agosti 17, mwaka huu.

Hatua hiyo imetokana na kuwepo kwa  maombi yaliyokuwa yamewasilishwa na upande wa utetezi unaowakilishwa na mawakili Nehemia Nkoko, Nestory Wandiba na Evodius Mtawala.

Mawakili hao, waliibua hoja ya kwamba haikuwa sahihi kwa mahakama kupokea hati ya mashtaka wakati washtakiwa wawili hawapo.

Hoja hiyo ilipingwa na Wakili Swai akidai kwamba mahakama ilishaikubali hati ya mashtaka na washtakiwa waliopo waliweza kusomewa na kuamriwa kesi itasikilizwa baada ya washtakiwa wengine kupatikana.

Washtakiwa hao wanakabiliwa na mashtaka 10 yakiwemo ya kula njama, kughushi, kuwasilisha nyaraka za kughushi,  kutoa maelezo ya uongo na utakatishaji fedha haramu.