Msafara msiba wa Mzee Majuto wasimama mara 16

Donge Tanga. Hatimaye safari ya kuelekea Donge Tanga kwa ajili ya kumpumzisha aliyekuwa nguli wa sanaa ya vichekesho Amri Athumani maarufu King Majuto imetimia ambapo takribani wananchi wa vijiji kumi na sita walikuwa barabarani usiku kwa ajili ya kutaka kuaga mwili huo.
Safari hiyo ambayo ilianzia katika ukumbi wa Karimjee ambapo mwili huo ulikuwa ukiangwa na baadae magari ya kusafirishia watu yaliongozana kupitia Barabara ya Bagamoyo,yalipofika kijiji kinachoitwa Mkata  mamia ya wananchi wa eneo hilo walisimama kando ya barabara wakisubiria mwili kwa hamu ili waweze kuuona.
Kijiji kilichofuata kilikuwa Kabuku,Kwe dizinga, Michugwani, Hale, Maguzoni,Kwabastola, Kibanda.
Vijiji vingine vilivyokuwa barabarani vinasubiria mwili ni Muheza,Lusanga,Mkanyageni,Pongwa,Majani Mapana,Mwamboni,kwa Minchi na Mabanda ya Papa.
Kila kijiji wananchi hao waliosimama barabarani walisikika wakimuombea kwa maombi ya dini zote na wengine wakilia kwa uchungu huku wakiita Baba na Babu
Wakizungumza na MCL Digital kwa nyakati tofauti,wanavijiji hao walisema:
"Huyu ni Mzee wetu jamani,tuko hapa toka saa kumi na mbili tunamsubiria tumuone tu,yaani namkumbuka sana marehemu kwa sababu alikuwa ni mchekeshaji ambaye tulikuwa tunajivunia katika kijiji chetu cha Kibanda," alisema mwanamke aliyejitambulisha kwa jina moja la Aziza.
"Dada usituone tuko hapa,sisi Mzee Majuto kwetu ni kama almasi,alikuwa anatujali sana,maana alikuwa akitoka Dar es Salaam lazima ashuke hapa Muheza kutusalimia,yaani alikuwa sio mtu wa majivuno daah" walisema Ally mkazi wa Muheza.