Yanga yaifyatua pacha wa Simba mabao 5-1

Yanga imecheza mchezo wake wa kwanza wa kirafiki dhidi ya timu ya Tanzanite Sport Academy na kuibuka na ushindi mkubwa wa mabao 5-1  lakini kocha wake Mwinyi Zahera akasema anataka mechi ngumu zaidi.

Katika mchezo huo ambao Zahera alichezesha vikosi viwili vilivyogawana dakika 45 Yanga ilionekana kuwa imara katika dakika 45 za kwanza.

Ikicheza soka la kasi Yanga ilimaliza dakika 45 za kwanza kwa kuongoza kwa mabao 4-1 mabayo yakifungwa na washambuliaji Heritier Makambo,Mrisho Ngassa na viungo Deus Kaseke,Emmaneul Martin na Pius Buswita.

Kocha Mwinyi Zahera aliwaanzisha kipa Benno Kakolanya akilindwa na mabeki Juma Abdul, Mwinyi Haji, Andrew Vincent 'Dante', Abdallah Shaibu 'Ninja.

Katika kiungo kikosi hicho kilichtengeneza sehemu kubwa ya ushindi huo kilikua na nyota Feisal Salum,Buswita,Raphael Daud,Ngassa,Kaseke huku mshambuiaji akiwa Makambo.

Mpaka mapumziko Yanga ilimaliza ikiongoza kwa mabao 4-1 yaliyofungwa na Ngassa,Buswita,Kaseke na Makambo huku lile la Tanzanite likifungwa na Omari Jaribu.

Kipindi cha pili Zahera alibadili kikosi kizima ambacho nacho licha ya kupoteza nafasi nyingi kiliambulia kutengeneza bao moja pekee likifungwa na Martin aliyetengenezewa nafasi nzuri na kiungo Edward Maka.

Kikosi hicho kilikuwa na nyota Klause Kindoki,Juma Mahadh,Gadiel Michael,Pato Ngonyani,viungo wakiwa Thabani Kamusoko,Jafary Mohamed aliyetolewa na kungia Maka,Said Juma,Yusuf Mhilu aleyetolewa na kuingia Martin wakati washambuliaji wakiwa Amissi Tambwe na Matheo Antony.

Akizungumzia mechi hiyo Zahera alisema amefankiwa kupata kipimo kizuri kwa wachezaji wake lakini bado ameomba kutafutiwa mechi ngumu zaidi kuweza kupima uboa wa wachezaji wake.

Zahera alisema endapo atapata mechi mbili na vikosi vigumu ataweza kujua ubora wa timu yake kabla ya kukutana na USM Alger ya Algeria.

"Hii ni mechi ya kwanza lakini sitaki kuzingatia chochote katika kilichotokea leo (jana) bado nahitaji mechi ngumu kama mbili kabla ya kukutana na USM Alger.

"Nataka kujua ubora zaidi kwa kuwa tumemaliza sehemu kubwa ya maandalizi lakini  sasa nataka kuangalia kipi kimeingia kiufundi ili tujue turekebishe wapi."