VIDEO: Simba wamiminika kuijaza Taifa

MWITIKIO wa mashabiki wa Simba kwenye tamasha la klabu hiyo la Simba Day umeonekana kuwa chanya kutokana na umati uliojitokeza kwenye Uwanja wa Taifa jijini leo.
Dalili za mashabiki hao kujazana uwanja wa Taifa zilianza kuonekana mapema kuanzia majira ya saa 2 ambapo mabasi yaliyowabeba yalianza kuonekana barabarani yakiwapeleka uwanjani hapo.
Mashabiki hao walianza kuingia uwanjani mnamo saa 4 asubuhi na wengi wao walikimbilia upande wa majukwaa ya Magharibi iliko skrini kubwa.
Hadi kufikia saa tano, sehemu kubwa ya viti vya majukwaa ya rangi ya kijani, bluu na machungwa ambayo yapo upande huo ilikuwa imejaa.
Hamasa ya mashabiki kuingia uwanjani oliongezeka zaidi pale Bendi ya Muziki wa dansi ya Twanga Pepeta ilipoanza kutumbuiza mnamo saa saba kasoro mchana.
Nje ya Uwanja wa Taifa, umati wa mashabiki umekuwepo hasa kwenye mageti wakiwahi kuingia uwanjani lakini pia wameonekana kwenye misururu mirefu pembezoni mwa Uwanja wa Uhuru na kwenye baadhi ya magari maalum yaliyoandaliwa kuuza tiketi za kuingilia uwanjani