MJIPANGE: Hawana huruma na mtu kabisa

HATUMWI mtoto dukani leo. Ukisikia mambo ni moto, basi ndio leo. Mabingwa wa soka Tanzania tayari wameshatua nchini wakitokea Uturuki walikokuwa wameweka kambi maalumu kwa ajili ya kujiandaa na msimu mpya wa Ligi Kuu Bara utakaoanza Agosti 18 kwa timu hiyo kuvaana na Mtibwa Sugar ya Manungu, Morogoro, pamoja na michuano mingine ikiwamo ya kimataifa.

Leo ni Simba Day na kikosi kizima kinatarajiwa kutambulishwa mbele ya mashabiki, sambamba na utambulishaji wa jezi mpya pamoja na burudani nyingine na yote hayo yatafanyika pale Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Mbali na mashabiki wa timu hiyo kupata fursa ya kununua jezi za timu yao, pia watashuhudia kikosi chao matata kabisa chini ya Kocha Mkuu, Mbelgiji Patrick Aussmes ambacho katika kunogesha siku hii maalumu ya Simba Day, watajitupa uwanjani hapo kuvaana na Asante Kotoko ya Ghana.

Hata hivyo, baada ya kumalizika kwa msimu uliopita wa Ligi Kuu Bara, Simba ilifanya usajili matata kwa kunasa mastaa wapya, ambao watakuwa na kazi ya kuthibitisha ubora wao mbele ya mashabiki wao kabla ya kuanza kwa purukushani ya kutetea taji lao.

Mwanaspoti limezungumza na mastaa hao na wamefunguka mengi huku wakiwataka mashabiki wa timu hiyo kutuliza mzuka.

MARCEL KAHEZA

Msimu uliopita 2017/18 , Keheza alikuwa moto akiwa na Majimaji ya Songea, akifumania nyavu mara 14, japokuwa Majimaji ilishuka daraja baada ya kushindwa kufanya vizuri.

Hata hivyo, mara tu baada ya msimu kumalizika, alinaswa na Simba na mshambuliaji huyo mwenye ndoto ya siku moja kuwa mfungaji bora wa Ligi Kuu Bara, amesema alikuwa anaisubiri kwa hamu siku ya leo ili kutambulishwa mbele ya mashabiki wa timu hiyo ambao, wamekuwa wakimfurahia tangu ajiunge na Simba. “Hii ni siku maalumu ambayo kama mchezaji naipa heshima yake, pia itakuwa siku nzuri ya kukutana na mashabiki ambao nategemea sapoti kubwa kutoka kwao,” anasema mshambuliaji huyo.

MOHAMMED RASHID

‘Mo’ ni jina lingine kwenye kikosi cha Simba litakalotambulishwa mbele ya maelfu ya mashabiki wa Simba.

Akifunguka kuhusu Simba Day, straika huyo wa zamani wa Tanzania Prisons amesema anaichukulia siku ya leo kama ya kula kiapo.

“Binafsi naitafsri hivyo kwa sababu itakuwa ni kama ufunguzi wa msimu mpya wa ligi na tutacheza mechi ya Ngao ya Hisani na Mtibwa Sugar. Naahidi sitawaangusha mashabiki wangu na Simba,” anasema MO.

ABDUL SELEMAN

Huyu ni kinda wa timu ya Taifa ya vijana chini ya miaka 20. Naye atakuwepo pale Taifa kutambulishwa baada ya usajili wake katika dirisha la usajili lililopita akitokea Ndanda FC ya Mtwara. Straika huyo ambaye alikuwa sehemu ya kikosi cha Serengeti Boys kilichofanya makubwa kule Gabon kwenye fainali za mataifa ya Afrika kwa vijana chini ya miaka 17, anajiona mwenye furaha ndani ya Simba na kuhusu Simba Day anafunguka.

“Sina mengi zaidi ya kusema tukutane pale Uwanja wa Taifa, lakini kikubwa nina furaha kuwa miongoni mwa wachezaji wa Simba,” anasema kinda huyo.

MEDDIE KAGERE

Kwa sasa ndio habari ya mjini unaambiwa. Tangu atue Bongo ameonyesha ni moto kwelikweli na timu pinzani lazima zijipange, la sivyo atawanyoosha.

Mashabiki wa Simba kwa sasa hawana presha kabisa kwenda uwanjani kuiangalia timu yao kwani, wana uhakika wa ushindi.

Kagere ameshatupia mabao manne kwenye michuano ya Kagame ambayo Simba ilimaliza nafasi ya pili na kuwa tumaini jipya klabuni hapo.

ADAM SALAMBA

Nyota wa zamani wa Lipuli FC ambaye awali alikuwa akisumbuliwa na majeraha ya kuchanika kwa nyama za paja. Hii ni mara yake ya kwanza kuwa kwenye kikosi cha Simba na atakuwepo kwenye utambulisho wa kikosi hicho kwenye siku hii maalumu ya Simba Day. Pale Simba ameanza na moto na ukitaka uuone moto wake, we fika tu pale Taifa na mfuatilie kwenye mechi za Ligi Kuu.

Tayari ameitumikia Simba kwenye michuano ya Kagame na kupachika mabao matatu, hana presha kabisa kwani mashabiki wa Simba wanamfahamu vyema tangu akiwa Lipuli.

PASCAL WAWA

Beki wa zamani wa Azam FC ya Chamazi jijini Dar es Salaam, Wawa ambaye anatajwa kuziba pengo la Juuko Murishid amewataka washambiki wa Simba kujitokeza kwa wingi Taifa.

“Tupo kwa ajili ya kuwapa burudani kabla ya kuanza kwa msimu kwa hiyo ni vyema wakajitokeza kwa wingi,” anasema beki huyo wa kati uraia wa Ivory Coast.

DEOGRATIUS MUNISH ‘DIDA’

Dida alijiunga na Simba akitokea Afrika Kusini kwenye klabu ya University of Pretoria FC ambayo alimaliza nayo mkataba.

Tayari ameshaitumikia Simba kwenye michuano ya Kombe la Kagame na leo atatambulishwa mbele ya maelfu ya mashabiki wa timu hiyo.

CLETUS CHAMA

Kiungo mpya wa Zambia, Chama ametua Simba kusaidiana na kina Jonas Mkude, Haruna Niyonzima kusongesha jahazi la Simba. Bado hajaonekana uwanjani kwani, alisajiliwa dakika za mwisho wakati kikosi hicho kikijiandaa kwenda kambini Uturuki. Chama alijiunga na Simba Julai 22, mwaka huu akitokea Lusaka Dynamos ya Zambia, lakini shughuli yake uwanjani imekuwa ikiwapa jeuri kinoma mashabiki wa Simba.