Bingwa wa Dunia mita 400 viunzi afariki dunia kwa ajali ya gari

Nairobi, Kenya. Bingwa wa zamani wa dunia, mita 400, kuruka viunzi, Mkenya Nicholas Bett, amefariki Dunia, baada ya kuhusika katika ajali mbaya ya gari iliyotokea leo Jumatano asubuhi katika barabata kuu inayopita Msitu wa Burnt, Kaunti ya Nandi.
Bett, ambaye alishinda mbio hizo katika mashindano ya Dunia, yaliyofanyika nchini China, Agosti 25, mwaka 2015, alikutwa na umauti wa ghafla asubuhi ya leo, baada ya gari lake, kupoteza muelekeo na kutoka barabarani kabla ya kutumbukia korongoni, karibu na eneo la Lessos, kwenye Barabara ya Eldoret- Kapsabet.
Kwa mujibu wa Mkuu wa Polisi wa Kaunti ya Nandi, Patrick Wambani, Mwanariadha huyo, ambaye alifariki dunia papo hapo na kwamba mwili wake umehifadhiwa katika chumba cha kuhifadhia maiti ya Hospitali ya kaunti.
Wambani alisema kuwa wakati wa ajali hiyo, Bett ambaye alikuwa sehemu ya timu ya Kenya, iliyomaliza katika nafasi ya kwanza katika mashindano ya Afrika yaliyomalizika Agosti 5, huko Assaba Nigeria, alikuwa anarudi Nyumbani (Nandi) akitokea Nairobi, baada ya kurejea nchini akitokea Nigeria.