Maria Sharapova apeta Rogers Cup

Montreal, Canada. Mcheza tenisi mahiri wa Russia, Maria Sharapova, amerejea katika kiwango chake bora baada ya jana kumng’oa Sesil Karatantcheva wa Bulgaria, katika michuano ya Rogers Cup.

Sharapova alimshinda Sesil Karatantcheva kwa seti mbili za 6-1, 6-2 ikiwa ni mara yake ya kwanza kushiriki mashindano ya Rogers Cup tangu mwaka 2014.

Naye mchezaji Eugenie Bouchard wa Canada anayeshika nafasi ya 129 kwa ubora duniani alishinda kwa 6-2, 6-4 Elise Mertens wa Ubelgiji.

Hata hivyo Bouchard, aliumia kidole gumba cha mguu na kuomba mchezo usimamishwe ili atibiwe na baadaye kumalizia mchezo huo huku akichechemea.

Katika mchezo uliochezwa mapema Jelena Ostapenko wa Lativia alishindwa kuwika mbele ya Mwingereza Johanna Konta alipochapwa kwa 6-7 (6), 6-1, 6-2.

Naye  Kiki Bertens wa Uholanzi alimshinda Carol Zhao wa Canada, akimchapa kwa 6-1, 6-2 wakati Petra Kvitova alimshinda Anett Kontaveit wa Estonia kwa 6-3, 6-4.

Aidha mchezaji Alison Van Uytvanck wa Ubelgiji alimshinda Sofya Zhuk wa Russia kwa 6-1, 6-2 huku Sorana Cirstea akimshinda Monica Niculescu kwa 3-6, 6-4, 6-4 ukiwa ni mchezaji uloiowakutanisha wachezaji wote kutoka nchini Romania.

Mcheza tenisi mahiri wa Ujerumani, Julia Goerges naye alimshinda Lucie Safarova kwa 2-6, 6-4, 6-3, huku Victoria Azarenka wa Belarus akimshinda Mfaransa Kristina Mladenovic kwa 6-0, 6-1 na Caroline Garcia alimshinda Magdalena Rybarikova wa Slovakia kwa 4-6, 6-1, 6-3.