VIDEO: Leo ndio leo Simba Day

Dar es Salaam. Wanachama na mashabiki wa klabu ya Simba leo wanatarajiwa kujitokeza kwa wingi katika tamasha la kila mwaka la klabu hiyo maarufu kama Simba Day.
Tamasha hilo limekuwa likifanyika Agosti 8 ya kila mwaka likiwa maalumu kwa ajili ya kuwakutanisha wanachama na mashabiki wa klabu hiyo ambao mwisho hupata fursa ya kuwatambua wachezaji wote watakaoitumikia Simba kwa msimu husika.
Klabu hiyo imekuwa na utaratibu wa kuialika moja ya timu kutoka nje ya nchi ambayo hucheza mechi na kikosi chao kwa ajili ya kuwapa burudani mashabiki wa Simba na mashabiki wa soka nchini kwa ujumla.
Simba imekuwa klabu pekee nchini hadi sasa kufanya tamasha makubwa linaloonekana kuwa ni kumbukizi ya kuanzishwa kwa klabu hiyo kongwe iliyoanzishwa tangu mwaka 1936.
Katika kuonyesha thamani na umuhimu wa siku hiyo, kuanzia Agosti mosi kumekuwa kukifanyika mambo mbali mbali ya kijamii iwe ni kwa wanachama kufanya usafi, kuwatembelea wagonjwa mahospitalini, kuvitembelea vituo vya kulea yatima na mengineyo.
Uongozi wa Simba ulipanga utaratibu huu ufanyike kwa wanachama na mashabiki wa klabu hiyo nchi nzima, lakini hilo bado halijapata upokezi mzuri kutoka kwa viongozi wa matawi ya mikoani.
Burudani ya soka
Kwa tamasha la Simba Day 2018, klabu hiyo imeialika timu kongwe ya Asante Kotoko kutoka nchini Ghana, ambayo leo ndiyo itakayotoa burudani kwa mashabiki wa soka nchini itakaposhuka dimbani kucheza na wenyeji wao Simba maarufu kama ‘Wekundu wa Msimbazi’.
Kikosi cha Asante Kotoko kiliwasili nchini jana asubuhi ambapo kilishuka kwenye uwanja wa ndege wa JKIA saa 3:00 asubuhi na kulakiwa na wenyeji wao tayari kwa mchezo wa leo.
Mchezo huo wa kirafiki dhidi ya Simba SC utakaopigwa kwenye uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam ndiyo hitimisho la tamasha la Simba Day kwa mwaka 2018.
Kutokana na aina ya usajili uliofanywa na Simba baada ya  dirisha la usajili la kiangazi kufunguliwe bila shaka mashabiki mashabiki watakaofika uwanjani watapata burudani ya aina yake.
Licha ya kwamba mabingwa hao wa Ligi Kuu Tanzania Bara wameendelea kuwa na wachezaji wao wote muhimu walioipa ubingwa msimu uliopita, lakini imeongeza wengine zaidi.
Wachezaji hao waliongezwa licha ya baadhi yao kuonekana katika michuano ya Kombe la Kagame lakini ndio watatambulishwa rasmi wakiwa na jezi watakazozitumia katika Ligi na michuano mingine.
Mbali ya Ligi Kuu Simba itashiriki Kombe la Shirikisho nchini pamoja na kuwakilisha nchi katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Wachezaji wapya wa Simba ni pamoja na kipa wa zamani wa Klabu hiyo, Deogratius Munishi ‘Dida’ aliyekabidhiwa jezi namba 32, beki wa zamani wa Azam FC, Pascal Wawa aliyekabidhiwa jezi namba 27 na mpiga mabao kutoka Rwanda, Meddie Kagere, ambaye atakuwa akivalia jezi namba 14.
Wachezaji wengine ni Adam Salamba, Mohamedi Rashid na Marcel Kaheza ambao walisajiliwa mapema pale tu dirisha la usajili lilipofunguliwa.
Mashabiki wa Simba leo watapata fursa ya kuwaona wachezaji hao pamoja na wale wa zamani walioing’arisha timu hiyo akiwemo nahodha John Bocco ‘Adebayor’, Mohamed Ibrahim, Shiza Kichuya, Mzamiru Yassini na wengine wengi.