Mkongwe El Hadary astaafu soka Misri

Cairo, Misri. Kipa mkongwe wa Misri, Essam El-Hadary, ambaye Julai mwaka huu aliweka rekodi ya kuwa mchezaji mkongwe zaidi kuwahi kucheza fainali za Kombe la Dunia, amestaafu rasmi soka la kimataifa.

El – Hadary mwenye miaka 45, ambaye katika kikosi cha Misri ametwaa mataji manne ya ubingwa wa Afrika alicheza mechi yake ya kwanza mwaka 1996 na ameitumikia nchi yake katika mechi 159.

Kipa huyo aliidakia Misri katika mechi ya mwisho hatua ya makundi na akaonyesha umahiri wake alipopangua penalti katika mchezo ambao walifungwa mabao 2-1 na Saudi Arabia.

"Baada ya kuidakia timu ya Taifa ya Misri kwa miaka 22 miezi minne na siku 12 sasa naona ni muda muafaka kwangu kutundika gloves zangu," alisema El- Hadary.