Mwingereza Katie abwagwa tenisi

Montreal, Canada. Mchezaji tenisi wa Uingereza, Katie Boulter ameng’olewa katika raundi ya kwanza ya mashindano ya Rogers Cup yanayoendelea mjini Montreal, Canada.

Katie mwenye miaka 22, alipoteza mchezo dhidi ya Lesia Tsurenko wa Ukraine na kuendeleza msimu mbaya ambapo mwaka huu aliaga mashindano ya Wimbledon katika raundi ya pili.

Katika mchezo wa juzi, Lesia mwenye miaka 29, alimshinda kirahisi kwa seti mbili za 6-4 6-2 akitumia dakika 85.

Katie aliingia uwanjani akiwa na matumaini ya kushinda ili kupanda viwango vya ubora wa tenisi duniani kwa kuingia katika 100 bora kwa mara ya kwanza katika historia yake.

Katika mchezo mwingine kigogo wa tenisi wa Marekani Venus Williams alishinda dhidi ya Caroline Dolehide seti 7-5 6-1 sawa na Karolina Pliskova aliyepata ushindi wa seti 6-4 6-4 alipovaana na Katerina Siniakova.

Venus mwenye miaka 38 anaonekana kurejea katika kiwango chake cha ubora wa tenisi akiwa na mataji saba ya Grand Slam, alipangiwa kucheza na mshindi wa mchezo kati ya Sorana Cristea na Monica Niculescu.