Kessy wa Yanga 'kazingua' tena nini?

Muktasari:

Mpango mzima ulikuwa hivi,  leo hii wachezaji wote wangefika mazoezini kujiandaa na mechi yao ya marudiano ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Gor Mahia ya Kenya, mchezo unaotarajiwa kupigwa mwishoni mwa mwezo huu.

Dar es Salaam: Nyota wa Yanga wameendelea na mazoezi asubuhi ya leo Jumatatu kwenye Uwanja wa Police College Kurasini jijini Dar es Salaam lakini kilichotokea huko, we acha tu.
Unajua iko vipi, jana Jumapili kilifanyika kikao cha nguvu katika Makao Makuu ya Klabu ya Yanga pale mitaa ya Jangwani kati ya uongozi wa timu pamoja na wachezaji.
Mpango mzima ulikuwa hivi,  leo hii wachezaji wote wangefika mazoezini kujiandaa na mechi yao ya marudiano ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Gor Mahia ya Kenya, mchezo unaotarajiwa kupigwa mwishoni mwa mwezo huu.
Wachezaji walitoka hapo wakiwa katika morali ya juu wakimaanisha kuwa kila kitu kitakwenda sawa na wanasahu yote ya nyuma.
Lakini cha kushangaza ni kwamba, Hassan Ramadhan 'Kessy' ambaye alikuwa ni miongoni mwa wachezaji 19 waliohudhuria mkutano huo wa jana na hakuonekana mazoezini .
Kessy ameungana na wachezaji wengine watano ambao pia hawakufika mazoezini, Kelvin Yondani 'Vidic', Andrew Vicente 'Dante', Benno Kakolanya, Haji Mwinyi na Ibrahim Ajibu.