Yanga ikubali kuna maisha baada ya Manji

Dar es Salaam. Yanga si shwari tena kuanzia ndani ya uwanja hadi nje, kila moja anatafuta mlango wa kutokea.

Maisha ndani ya Yanga yamebadilika kwa haraka tangu aliyekuwa mwenyekiti wao, Yussuf Manji alipowekwa ndani na baadaye kutangaza kujiuzulu nyadhifa hiyo.

Tangu wakati huo Yanga imekuwa na maisha ya kusuasua kwa timu hiyo kupata matokeo mbaya ndani ya uwanja hadi kupoteza ubingwa wao wa Ligi Kuu Bara kwa watani zao Simba.

Hii ni mara ya kwanza kwa zaidi ya miaka 10 Yanga haitoshiriki mashindano ya Ligi ya Mabingwa wala Kombe la Shirikisho Afrika.

Jinamizi la kuondoka kwa Manji bado limeendelea kuitafuna timu hiyo kiasi cha msimu huu kuwapoteza wachezaji wake nyota Donald Ngoma, Obrey Chirwa pamoja na makocha George Lwandamina, Shadrack Nsajigwa wote wameondoka.

Pia, Katibu Mkuu wa Yanga, Charles Mkwasa. Mabingwa hao wa kihistoria wapo kwenye mgogoro na beki wa Kelvin Yondani, Ramadhan Kessy, Andrew Vicent wanaodai fedha zao za usajili ili kusaini mikataba mipya.

Matatizo hayo yamechangia timu hiyo kufanya vibaya katika mechi zake za hatua ya makundi ikiwa imefungwa USM Algers 4-0, Gor Mahia 4-0 na kulazimisha suruhu nyumbani na Rayon.

Katika kujaribu kuzima moto huo wa matatizo baadhi ya wadau wa Yanga wamemleta kocha Mwinyi Zahera kuchukua mikoba ya Lwandamina lakini bado kuna fukuto linaendelea.

Hata hivyo ujio wa kocha huyo Zahera umekosa nguvu kutokana na Mkongo huyo kukosa vibali vya kufanya kazi nchini hivyo muda mwingi amekuwa akikaa jukwaani.

Mbali ya hilo pamoja na Yanga kuwa na udhamini wa Sh950 milioni kutoka SportPesa kwa mwaka bado wachezaji wake wanadai mishahara  jambo linalofanya wagome kufanya mazoezi.

Yanga wamsahau Manji

Matatizo hayo na mengine yanayoikabili Yanga kwa sasa yaweza kuisha iwapo uongozi wa klabu hiyo utakubali kuna maisha baada ya Manji.

Viongozi wa Yanga wakiongozwa na makamu mwenyekiti, Clement Sanga pamoja na mashabiki wao, bado hawajaamini kwamba klabu hiyo inaweza kuishi bila ya Manji.

Maisha ya kumtegemea Manji yameifanya klabu hiyo kushindwa kufikia uamuzi sahihi wakati wa mkutano mkuu uliofanyika hivi karibuni.

Ili Yanga irudi katika mstari ni lazima Sanga na timu yake waitishe uchaguzi mkuu haraka ili wapate mwenyekiti mwingine atakayekuja na mipango ya kuinusuru timu na hali ya sasa.

Pia, kuondoka kwa Manji na ukata wanaopitia iwe somo kwao katika kutengeza mfumo bora wa kuifanya klabu hiyo kujiendesha kibiashara na kuachana na kutegemea mfuko wa mtu binafsi. Waswahili wanasema ‘Mtegemea cha ndugu hufa masikini.’