Yanga majanga kila kona

Wachezaji wa Yanga wamegomea mazoezi ya leo Ijumaa, huku benchi la Ufundi wakibaki na mshangao kwenye Uwanja wa Polisi Kurasini jijini Dar es Salaam.

Akizungumza na MCL Digital, Meneja wa Yanga, Salehe Hafidhi amethibitisha kwamba wachezaji watatu wageni ndio waliojitokeza kwenye mazoezi ya leo asubuhi.

Wachezaji hao ni Deus Kaseke, Mrisho Ngassa na Heritier  Makambo ambao wote hao wamesajili kweye dirisha la msimu huu.

Hafidhi alisema sababu kubwa ambazo amezipata juu ya wachezaji hao kugoma ni kutokana na madai yao ya fedha.

Aliongeza kuwa ameshawasilina na uongozi ili kujua nini cha kufanya isipokuwa benchi la ufundi litaendelea na ratiba yake ya mazoezi kama kawaida kesho Jumamosi Asubuhi.

Timu hiyo inapita katika kipindi kigumu kutokana na kuwepo na taarifa kwamba inakabiliwa na ukata.

Jumatano wiki hii kikosi cha Yanga kiliambulia kipigo cha mabao 4-0 kutoka kwa Gor Mahia katika mchezo wa kimataifa wa Kombe la Shirikisho Afrika.