CECAFA 2018: Harambee Starlets washindwa kuzuia kasi ya Uganda

Nairobi. Timu ya taifa ya Kenya ya wanawake, 'Harambee Starlets' imeshindwa kuzuia kasi ya Crested Cranes ya Uganda katika mchezo wa kwanza wa michuano ya Cecafa 2018, yaliyoanza leo katika uwanja wa Nyamirambo, jijini Kigali, nchini Rwanda.

Starlets inayonolewa na David Ouma iliingia katika mchezo huo uliomalizika muda mfupi uliopita wakiwa na uhakika wa kuendeleza ubabe dhidi ya majirani zao hao, lakini wakajikuta wakijikaba wenyewe wakiwaacha Cranes kucheze mpira kwa raha zao.

Tofauti na ilivyokuwa katika michezo ya awali iliyokutanisha pande hizi mbili, Uganda walionekana kuwa imara na wenye kiu ya kupata ushindi wakicheza mpira wa kasi ambapo katika dakika ya saba ya kipindi cha kwanza, Lilian Mutuuzo, aliweka mpira wa kona kambani na kumuacha Poline Atieno akishangaa tu.

Baada ya kufungwa bao hilo, Starlets walizinduka na kufanya na mashambulizi kadhaa langoni mwa Uganda, lakini juhudi zao ambazo ni pamoja na mabadiliko yaliyofanywa na David Ouma ya kuwaleta Esse Akida na Martha Amunyolete, kuchukua nafasi ya Terry Engesha na Mercy Achieng, hazikuzaa matunda.

Katika dakika ya 15, Neddy Atieno alifunga bao lakini mwamuzi akaonesha alikuwa ameotea, tukio hili likija dakika chache baada ya Starlets kunyimwa penalti. Dakika mbili baadae, shuti la Mwanahalima Adam liligonga mwamba.

Kipindi cha kilianza na kuendelea kwa kasi ileile ambapo pande zote zilishambuliana kwa zamu lakini hadi dakika 90 zinamalizika, sio Crested Cranes wala Harambee Starlets waliofanikiwa kupata bao. Mwisho wa siku Uganda wakatoka uwanjani kifua mbele.

Kikosi cha Harambee Starlets:

Poline Atieno, Lilian Adera, Dorcas Shikobe, Elizabeth Ambogo, Wendy Achieng, Cheris Avilia, Cynthia Shilwatso, Mercy Achieng (Martha Amunyolete), Mwanahalima Adam, Neddy Atieno, Terry Engesha (Esse Akida)

Kikosi cha Crested Cranes:

Ruth Aturo, Viola Namuddu, Grace Aluka, Shadia Nankya, Yudaya Nakayenze, Tracy Akiror (nahodha), Lilian Mutuuzo, Phiona Nabbumba, Ziana Namuleme, Juliet Nalukenge, Norah Alupo (Winnie Babibrye)