Lyon yaipa masharti magumu Liverpool

Lyon, Ufaransa. Klabu ya Liverpool, imetakiwa kukamilisha haraka uhamisho wa kiungo mshambuliaji Nabil Fekir, vinginevyo inaweza kumkosa.
Klabu ya Lyon imeipa Liverpool muda wa mwisho kukamilisha uhamisho na ikishindwa itamuondoa sokoni mchezaji huyo na kumjumuisha katika kikosi kinachojiandaa na msimu mpya wa Ligi Kuu Ufaransa.
Fekir aliyecheza Lyon mechi 115 na kufunga mabao 45, alikaribia kutua Liverpool katika usajili uliopita, lakini uhamisho wake ulikwama dakika za mwisho kutokana na ukubwa wa ada Pauni 53 milioni.
Rais wa Lyon, Jean-Michel Aulas, alisema Liverpool isipokamilisha uhamisho huo mapema, itamlazimisha mchezaji huyo kujiunga na wenzake wanaoanza maandalizi ya msimu mpya wa Ligi.
Fekir aliyeng’ara katika fainali za Kombe la Dunia licha ya kucheza akitokea benchi, alisisitiza anataka kutua Makao Makuu Anfield alikoahidiwa mkataba wa miaka mitano na mshahara wa Pauni 120,000 kwa wiki.