Idadi ya mechi Ligi Kuu yaibua mjadala

Muktasari:

Timu zilizopanda Ligi Kuu ni African Lyon, KMC, JKT Tanzania, Alliance United (Mwanza), Biashara United (Mara) na Coastal Union ya Tanga.

Dar es Salaam. Ongezeko la idadi ya mechi za Ligi Kuu Tanzania Bara, msimu ujao limewaibua wachezaji wanaoshiriki mashindano hayo.
Ligi Kuu msimu ujao itakuwa na timu 20 badala ya 16 na kila moja itacheza mechi 38 kulinganisha na 30 za msimu uliopita
Mwananchi limezungumza na na baadhi ya wachezaji ambao wametoa maoni kuhusu mwelekeo wa Ligi Kuu msimu ujao.
Beki wa Mbao David Mwasa, alisema mechi 38  zitawapa  uzoefu  wa ligi na ushindani utaongezeka ingawa watakabiliwa na uchovu.
“Timu zote zingekuwa imara kiuchumi kwa kuwawezesha wachezaji  kusafiri kwa ndege, ongezeko la mechi hizo ungekuwa mzuri wengi wangepata nafasi ya kucheza, lakini kwa usafiri wa kutumia basi utatuumiza na kutufanya tuchoke,”alisema Mwasa.
Mshambuliaji wa Azam Yahya Zayd alisema watapata faida ya kuimarika kiushindani, kuwajengea uzoefu wa kucheza muda mrefu na kumpa kocha muda wa kutosha kutambua uwezo wa kila mchezaji.
Zayd alisema endapo mchezaji  hatakuwa makini kujiandaa kikamilifu atapata maumivu ambayo yatamuweka nje muda mrefu kwa kulazimisha mwili kucheza idadi nyingi ya mechi.
“Kuna faida na hasara katika ujio wa mechi 38, kikubwa ni mchezaji mwenyewe kujiongeza na kujua namna ya kukabiliana na jambo hilo, sio kufanya mazoea ambayo yatamfanya ashindwe kufikia ndoto yake,”alisema mchezaji huyo.
Beki wa Simba, Ally Shomari  aliutazama ujio wa mechi 38 ni fursa kwa kuwa utatoa nafasi kwa kila mchezaji kucheza na kupata uzoefu.
“Mechi nyingi zina faida kwetu zinampa fursa mchezaji kucheza lakini lazima afanye maandalizi ya  kutosha ili kuwa fiti kwa mashindano. Hasara yake ni kuchoka na changamoto ya viwanja visivyokuwa na ubora hasa vya mikoani,” alisema beki huyo wa zamani wa Mtibwa Sugar.
Kwa upande wake mshambuliaji wa Yanga, Emmanuel Martin alisema mechi 38 ni fursa kwa wachezaji wote  kupata nafasi ya kuonyesha uwezo wao.
“Mchezaji anapocheza mechi nyingi inamjengea kujiamini, uzoefu na kujua zaidi sheria kwangu naona kuna faida kwa ongezeko la mechi kwa kuwa itawasaidia wachezaji wote kupata nafasi ya kucheza,” alisema Martin.
Timu zilizoshuka na msimu ujao zitacheza Daraja la Kwanza ni Njombe Mji kutoka Njombe na Majimaji ya Songea 
Timu zilizopanda Ligi Kuu ni African Lyon, KMC, JKT Tanzania, Alliance United (Mwanza), Biashara United (Mara) na Coastal Union ya Tanga.