VIDEO: Yanga yaishika pabaya Gor Mahia

Nairobi. Licha ya kuwakosa mabeki tegemeo Kelvin Yondani na Hassani Kessy, Yanga imesema haitakubali ‘kufa’ ugenini katika mchezo wa leo dhidi ya Gor Mahia.

Yondani na Kessy wamebaki Dar es Salaam kutokana na sababu binafsi. Yanga inatupa karata yake leo saa moja usiku katika mchezo wa tatu wa Kombe la Shirikisho Afrika kwenye Uwanja wa Kasarani, Nairobi jijini hapa.

Yanga iliwasili juzi na kufikia Hoteli ya The Luke iliyopo katikati ya Nairobi na jana ilifanya mazoezi usiku kwenye Uwanja wa Kasarani utakaotumika katika mchezo wa leo.

Kocha wa Yanga, Mwinyi Zahera alisema hana hofu ya kuwakosa Yondani na Kessy katika mchezo huo kwa kuwa ana kikosi kipana na wapo wachezaji wa kuziba nafasi zao.

“Nimeongea vizuri na wachezaji niliokuwa nao ingawa kukosekana kwa baadhi ya wazoefu inaweza kutuweka katika mazingira magumu, lakini hamna shida tumejipanga vizuri,” alisema.

Zahera alisema ameiona Gor Mahia, inaundwa na wachezaji wengi wazoefu ambao aliwaona katika mashindano ya Sport Pesa yaliyofanyika hapa na Kombe la Kagame yaliyomalizika Julai 13 Dar es Salaam.

Kocha huyo alisita kutaja mfumo atakaotumia katika mchezo huo zaidi ya kusema ana matumaini utawawezesha kuibuka na ushindi dhidi ya wenyeji wao Gor Mahia.

Alisema Yanga ilikuwa na upungufu katika maeneo madogo ambayo ameyafanyia kazi akiangalia kasoro zilizojitokeza katika mechi mbili zilizopita.

Kocha huyo alidokeza kuwa anaweza kukosekana katika benchi la ufundi kutokana na vibali vyake vya kufanyia kazi kutoka CAF kutokamilika.

Zahera anatarajiwa kuwatumia Ibrahim Ajibu na Amissi Tambwe katika safu ya ushambuliaji ambao wana uzoefu wa kutosha kwenye mashindano ya kimataifa. Pia wamo akina Juma Mahadhi, Emmanuel Martin na Pius Buswita.

Akizungumza na gazeti hili kocha wa Gor Mahia, Dylan Kerr alisema hautakuwa mchezo rahisi kwao kwa kuwa idadi kubwa ya wachezaji wake wamechoka baada ya kucheza mechi nyingi mfululizo za mashindano.

Kerr alisema wachezaji wana uchovu baada ya kushiriki mashindano ya Kombe la Kagame na kushika nafasi Gor Mahia.

Yanga haina rekodi nzuri inapocheza na Gor Mahia, katika mechi tatu walizocheza imefungwa mara mbili na kutoka sare mchezo mmoja.

Mwaka 1996 Yanga na Gor Mahia zilitoka sare ya bao 1-1 katika Kombe la Kagame kabla ya kuchapwa mabao 4-0 katika mchezo wa kusaka mshindi wa tatu. Mwaka 2015 Yanga ililala mabao 2-1 katika mashindano hayo.

Yanga ilianza mashindano kwa kulizwa mabao 4-0 na USM Alger kabla ya kutoka suluhu na Rayon Sports, Dar es Salaam.