Ya msimu uliopita yasijirudie tena ratiba mpya Ligi Kuu 2018-2019

Muktasari:

Wadau wa soka wana hamu kubwa ya kutaka kuiona ratiba hiyo mpya itakuwa imepangwa vipi, lakini kubwa ni kwa makocha, wachezaji na hata mashabiki kutaka kujua timu zao zitaanzia wapi na kuishia wapi ili zijipange.

BODI ya Ligi Kuu (TPLB) kesho Jumatano inatarajia kuianika ratiba ya Ligi Kuu Bara msimu wa 2018-2019, hii ikiwa ni baada ya kuahirisha kuitangaza jana Jumatatu.

Wadau wa soka wana hamu kubwa ya kutaka kuiona ratiba hiyo mpya itakuwa imepangwa vipi, lakini kubwa ni kwa makocha, wachezaji na hata mashabiki kutaka kujua timu zao zitaanzia wapi na kuishia wapi ili zijipange.

Mwanaspoti kama wadau wakubwa wa michezo hususan soka, tunaamini huenda ratiba hiyo ambayo kwa hakika imechelewa kutolewa, itakuwa imepangwa vyema na kuandaliwa kulingana na kalenda na mechi za mashirikisho ya kimataifa.

Hatutarajii kuona ratiba itakayotangazwa kesho hata kama ni ya awali, mbele ya safari inakuwa na vikwazo na kupanguliwa kila mara kwa kuingiliana na mechi za kimataifa ama kalenda za Mashirikisho ya Soka Afrika (CAF) ama la Dunia (FIFA).

Tunaamini Wajumbe wa TPLB pamoja na wale wa Kamati ya Mashindano ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kabla ya kuitengeneza ratiba hiyo walikaa chini na kuangalia jinsi ya kufuta dosari zilizosababisha rariba iliyopita kuyumba.

Kwa wanaokumbuka msimu uliopita licha ya ahadi tamu ya mabosi wapya wa TFF kwamba ratiba ya ligi haitapanguliwa bila sababu za maana, hali ilikuwa tofauti kwa kushuhudiwa ikipanguliwa ovyo kiasi cha kuchusha.

Msimu uliopita mara baada ya ligi kuanzwa kwa kuchezwa mechi za ufunguzi, ligi ilisimama kupisha mechi za kirafiki ambayo TFF na TPLB walipaswa kujua mapema na kuipanga ratiba yao kiufundi ili kuondoa vidole vya lawama kama walivyopata.

Kwa kuwa mtu hujifunza kutokana na makosa, ni wazi lililojitokeza kwenye ratiba ya msimu uliopita kwa ligi kusimama na kupanguliwa ovyo kiasi cha kuwakera mashabiki wanaopenda kwenda viwanjani, hayatajirudia tena safari hii.

Panga pangua ya ratiba mara kwa mara, hufanya ligi ipoteze mvuto na msisimko sambamba na kuwapunguzia mzuka wachezaji hasa kwa timu zinazofanya vizuri katika mechi zao.

Tunaamini TPLB na TFF kwa ujumla wamejipanga vyema na kuiandaa rariba ya msimu ujao kisomi na inayoendana na mazingira ya ongezeko la timu 20 zitakazoshiriki ligi hiyo, pia ni ratiba itakayotoa usawa kwa klabu zote.

Mwanaspoti linaamini wasimamizi wa ligi ni wasikivu na wamesikilia kilio cha muda mrefu cha mashabiki na wadau wa soka kwa jumla zikiwamo klabu, makocha wao, viongozi na hata wachezaji juu ya kero za panga pangua za ratiba ya Ligi Kuu Bara.

Itashangaza kama yale yaliyojitokeza kwenye ratiba ya msimu uliopita ambayo yalipigiwa kelele na kulalamikiwa yatajitokeza kwenye ratiba ya msimu huu, kama hilo litakuwepo basi itaonyesha TPLB na TFF hawajifunzi kutokana na makosa.

Kama hawajifunzi ni wazi ama wanadharau maoni na ushauri wa wadau wa soka au hawajui walifanyalo katika usimamizi wa soka letu kwa vile haiwezekani tatizo hilo hilo linalopigiwa kelele linajirudia kila msimu. Haipendezi. Haivutii.

Hivyo tunaamini ratiba inayoenda kutangazwa kesho Jumatano itakuwa ni yenye kujibu na kuziba mashimo yote yaliyokuwapo tangu enzi za utawala wa Leodegar Tenga na Jamal Malinzi juu ya panga pangua isiyoisha ya ratiba ya Ligi Kuu.

Pia tunaamini ratiba hiyo haitakuwa inazibeba baadhi ya timu na kuziumiza nyingine katika mfuatano wa mechi zao kwa nia ya kuifanya ligi iwe tamu na yenye kuvutia kiasi itachangia kuwavutia wadhamini zaidi wa kuja kuiongezea thamani.

Ubora wa ratiba utazifanya timu kutokuwa na lawama zozote baada ya matokeo na hivyo kuifanya ligi inoge wadau na mashabiki wakiamini kila kitu kilipangwa vizuri na ndio maana timu zinachuana bila tatizo.

Kama TPLB na TFF itarejea kuitangaza ratiba ambayo itakuwa inabadilika kila mara kama kinyonga na yenye kuzipendelea na kuziumia timu nyingine, ni wazi mvuto, msisimko na ushindani wa ligi ukapungua hata ligi haijaanza.

Hili lazima liepukwe hata kama huenda tumechelewa kutoa ushauri huu mapema, ila tunaamini zile kelele ambazo tumekuwa tukizitoa siku za nyuma sambamba na zile za wadau wengine, TPLB na TFF wamezingatia na kila kitu kitakuwa sawa.