Beki Yanga atua Singida United

BEKI wa zamani wa Yanga, Rajab Zahir anatarajia kusaini mkataba na Singida United muda wowote kuanzia sasa baada ya kufikia makubaliano na uongozi wa klabu hiyo.
Zahir aliyewahi kukipiga Stand United, Mbeya City na Ruvu Shooting usajili wake kwenda Singida United ulianza kutajwa tangu dirisha dogo la usajili msimu uliopita baada ya kocha Hans Pluijm kumpendekeza.
Singida inamhitaji beki huyo wa kati ili kwenda kuwapa changamoto nyota wao Kennedy Juma na Malik Antir. Antir hata hivyo inasemekana ataachwa.
Habari za uhakika ilizopata Mwanaspoti zinasema mazungumzo kati yao beki huyo na viongozi yamekamili kilichobaki ni kumpa mkataba ambapo imetajwa kuanzia leo Jumanne wanaweza kukamilisha mchakato huo.
"Ni kweli tunamsajili na kila kitu kipo safi, tunasubiri hatua ya mwisho ambayo ni kusaini mkataba, Zahir ni mchezaji mzuri na tangu msimu uliopita tulimuhitaji lakini alikuwa amesaini Ruvu Shooting hivyo tusingeweza kuingilia usajili wao." chanzo toka Singida kiliidokeza Mwanaspoti.
Zahir aliposakwa alisema; "Sina mkataba na timu yoyote baada ya kumalizana na Ruvu, nataka changamoto ya timu nyingine na kuna timu nazungumza nazo."